1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kilabu ya Hoffenheim yaendelea kuwa kitisho Bundesliga

4 Novemba 2008
https://p.dw.com/p/FlBu
Mshambuliaji wa Hoffenheim kijana Demba Ba ,akishangilia baada ya kufunga bao dhidi ya Bochum.Picha: AP

Katika ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga ambayo inaendelea leo (Jumamosi) kilabu ya Hoffenheim inayoongoza ligi hiyo itakua ikitafuta ushindi wake wa tano mfululizo itakapoumana na Karlsruhe huku mabingwa watetezi Bayern Munich wakianza kuweka shinikizo.Bayern wataumana na Arminia Bielefeld wakiwa pointi 4 nyuma ya Hoffeheim iliopanda daraja msimu huu na kuzusha maajabu.Timu hiyo wachezaji chipukizi ambao hadi sasa wamekua wakisakata dimba safi na kuwavutia wengi.

Kwengineko Hertha inaumana Werder Bremen, Schalke itachuana na Cottbus ambapo Stuttgart itatona jasho na FC Cologne. Hapo kesho itakua zamu ya Dortmund kupimana nguvu na Bochum na Borussia Monchengladbach ikiwa nafasi moja juu kutoka mkiani inacheza na Frankfurt. Bila shaka uchambuzi wa msimamo na matokeo ya Bundesliga utaweza kuusikia katika makala ya michezo mwishoni mwa Juma jumatatu jioni.

Taarifa nyengine za kandanda -liyekua mlinda mlango wa timu ya taifa ya Ujerumani na kilabu maarufu ya Uingereza Arsenal Jens Lehmann anataka kubakia katika ligi kuu Bundesliga kuakamlisha miaka 40 hapo mwakani akiendelea kucheza katika kilabu ya Stuttgart.

Lehmann ambaye atatimia umri wa miaka 40 tarehe 10 mwezi huu wa Novemba , anataka kuendelea na kilabu hiyo, licha ya kwamba kuna fununu mlinda mlango wa zamani Tim Hildebrand anayecheza Valencaia ya Uhispania wakati huu anapanga kurudi Stuttgart. Aidha Lehmann aliyestaafu kuichezea timu ya taifa mwezi Agosti mwaka huu baada ya kujiunga na Stuttgart kutoka Arsenal alikocheza miaka 5, amesema pia angependa kuwemo katika kikosi cha Ujerumani itakapoumana na Engaland katika mechi ya kirafiki tarehe 19 mwezi huu katika uwanja wa Olimpik wa Berlin.

Mchezaji huyo anakumbusha kipindi chjake cha kusisimua akiwa na timu ya taifa katika uwanja huo wa Olimpik Berlin Juni 30,2006 wakati wa mashindano ya kombe la dunia alipookoa mikwaju miwili ya Penalty dhidi ya Argentina baada ya kumaliza dakika 120 bila ya kupatikana mshindi. Umahiri wake ukaisogeza Ujerumani hadi nusu fainali.

Alisema angependa kucheza dhidi ya England kukumbuka miaka mingi aliyocheza dimba mjini London. Kocha wa Ujerumani Joachim Loew anatarajiwa kutangaza kikosi chake kwa ajili ya pambano hilo la kirafiki na England wiki ijayo.

Ubondia:

Bondia wa Urusi Alexander Povetkin amejiondoa katika pambano la mwezi Desemba dhidi ya bingwa wa uzani wa juu katika shirikisho la ndondi duniani IBF na Shirika la ndondi WBO Vladimir Klitschko wa Ukraine. Meneja wa Povetkin alisema bondia huyo hatokua kwenye matibabu yoyote lakini pambano Desemba 13 katika mji wa Ujerumani wa Mannheim hilo bila shaka , halitofanyika. Mrusi huyo mwenye umri wa miaka 29 ameshinda mapambano 16 yakiwemo 12 ambapo alimaliza udhia mapema yaani Knockout, ikiwa tangu alipogeuka bondia wa kulipwa 2005 baada ya mafanikio kama bondia wa ridhaa ikiwa ni pamoja na ushindi wa medali ya dhahabu katika uzito wa juu kwenye michezo ya olimpik 2004 mjini Athens Ugiriki.

Mshauri wa Klitschko mwenye umri wa miaka 32 , Shelly Finkel hata hivyo amesema bondia wake atapigana siku hiyo na wamo katika kumatafuta bondia mwengine atakayejaza nafasi ya Povetkin. Vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti kwamba miongoni mwa wanaotajwa kuwemo katika orodha hiyo ni pamoja na bingwa wa zamani Mrusi Oleg Maskaev na Mmarekani Hasim Rahman.

Riadha:

Bingwa wa zamani wa mbio za masafa mafupi kwa wanawake Marion Jones wa Marekani amekiri kwamba kutumia kwake madawa ya kuimarisha misuli na kuhukumiwa kifungo kwa udanganyifu kuhusu kadhia hiyo ni mambo yaliohujumu na kufuta mafanikio yake katika michezo ya Olimpik. Mwanariadha huyo pia alikutikana na hatia ya kudanganya kuhusu kitendo cha kugushi hundi ya fedha kilichomhusu mpenzi wake wa zamani na bingwa wa zamani wa mbio za mita 100 wanaume Tim Montgomery.Jones aliyasema hayo katika kipindi cha mahojiano cha Winfrey Oprah mmoja kati ya waongozaji wa vipindi maarufu vya burudani nchini Marekani.

Mwanariadha huyo wa zamani Jones ambaye alitoka gerezani mwezi uliopita baada ya kutumikia kifungo cha miezi sita kwa kuwadanganya waendesha mashtaka wa serikali juu ya matumizi yake ya madawa ya kuimarisha misuli yaliopigwa marufuku, alipokonywa na kamati ya olimpik ya kimataifa IOC, medali zote tatu za dhahabu na mbili za shaba alizoshinda wakati wa michezo ya Olimpik ya Sydney Australia.

Akiulizawa juu ya kadhia hiyo Jones aliungama kwamba alikua anajua anachofanya na aliamua tu kudanganya ili kuficha ukweli. Wakati wa mahojiano hayo alitokwa na machozi alipokua akiisoma barua aliyowaandikia watoto wake, wakati alipokua gerezani. Akatamka"ninaamini kwamba sababu ya kutenda kosa lile na mengineyo baadae, ilitokana na kutojipenda mwenyewe vya kutosha kuweza kuwa mkweli na muaminifu."

Naye Bingwa wa olimpik wa mbio za nyika marathon Naoko Takahashi kutoka Japan ambaye ndoto yake ya kutamba ilitoweka aliposhindwa kufuzu kwa ajili ya michezo ya olimpik ya Athens na Beijing ameamua kustaafu. Takahashi mwenye umri wa miaka 36 aliipatia Japan medali ya kwanza ya dhahabu ya Olimpik katika mbio za marathon kwa wanawake aliposhinda katika michezo ya Sydney mwaka 2000. Pia aliweka rekodi ya dunia ya marathon 2001 ya muda wa saa 2 dakika 19 sekunde 45.

Na Rais wa kamati ya kimataifa ya oölimpik IOC Jacques Rogge amethibitisha kwamba atagombea tena wadhifa huo kwa kipindi cha pili. Rogge mwenye umri wa miaka 60 na raia wa Ubeligiji alisema hayo katika taarifa yake Alhamisi akidhibitisha ile ya awali iliotolewa na kamati hiyo wiki iliopita.Tangu achaguliwe kwa kipindi cha miaka minane 2001, Rogge sasa atakua tu na haki ya kuiongoza asasi hiyo ya michezo kwa miaka minne zaidi.