1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tahadhari kubwa ya usalama yawekwa nchini Uingereza.

Mohamed Dahman1 Julai 2007

Serikali mpya ya Uingereza imeweka kiwango chake cha tahadhari dhidi ya ugaidi katika kiwango cha juu kabisa kufuatia majaribio matatu ya kuripua mabomu mawili yakiwa yamefanyika mjini London na la tatu katika uwanja wa ndege wa Glasgow huko Scotland.

https://p.dw.com/p/CB38
Mripuko kwenye mlango wa kuingilia uwanja wa ndege wa Glasgow.
Mripuko kwenye mlango wa kuingilia uwanja wa ndege wa Glasgow.Picha: AP

Hapo jana gari aina ya jeep lilibamizwa na lango la kuingilia kwenye uwanja huo na kuripuka moto.Watu wawili wamekamatwa mmoja akiwa ameunguwa vibaya sana.Polisi imesema bila ya kufafanuwa kwamba mtu huyo alikuwa na kifaa kwenye mwili wake.

Uwanja wa ndege wa Liverpool pia umefungwa.Polisi imesema imewakamata watu wengine wawili wakiwa kwenye barabara kuu kaskazini mwa Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown ambaye amechukuwa wadhifa huo kutoka kwa Tony Blair hapo Jumatano ameitisha mkutano wa kamati kuu ya usalama nchini Uingereza kujadili namna ya kukabiliana na mtihani wake wa kwanza wa uongozi.

Brown amewataka wananchi wote wa Uingereza kuwa macho na anawataka waunge mkono polisi na maafisa wa serikali katika maamuzi magumu ambayo itabidi wafanye. Amesema anatambuwa kwamba wananchi wa Uingereza watakuwa kitu kimoja.shupavu na imara.

Mshauri wa usalama wa Brown ambaye ni mkuu wa polisi wa zamani John Stevens amesema kuhusika kwa kundi la Al Qaeda katika njama hizo bado hakukuweza kuthibitishwa lakini amesema matukio hayo yanaonyesha kupamba moto kwa wanamgambo wa itikadi kali za Kiislam.

Polisi ya Uingereza imekuwa ikizipekua nyumba kadhaa karibu na uwanja wa ndege wa Glasgow.

Nchini Marekani usalama umeimarishwa katika viwanja vya ndege na abiria wameelezwa kwamba safari zao huenda zikacheleweshwa.

Hata hivyo waziri wa usalama wa ndani Michael Chetoff amesema kiwango cha hali ya tahadahari nchini humo kinabakia bila ya kubadilika lakini usalama umeimarishwa kwenye viwanja vya ndege wakati nchi hiyo ikielekea katika sikukuu ya Siku ya Uhuru nchini humo hapo Julani nne.