1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tai wa Nigeria wavunjwa mabawa na Mafarao

13 Januari 2010

Mabingwa watetezi Mafarao wa Misri jana walianza vyema safari yao ya kuutwaa kwa mara ya tatu mfululizo uchampion huo, kwa kuikandika Nigeria mabao 3-1, huku Mamba wa Msumbiji na Benin wakilazimishana sare ya mabao 2-2.

https://p.dw.com/p/LUNd
Kombe la mataifa ya Afrika, Angola 2010Picha: AP

Misri ambayo imeshindwa kufuzu kwa fainali za dunia nchini Afrika Kusini, ilionekana kana kwamba ingeondoka patupu uwanjani hiyo jana, baada ya kuruhusu kombora la mshambuliaji anayechezea klabu ya  ligi ya Ujerumani Bundesliga,Hoffenheim Chinedu Ubasi katika dakika ya 12 tu ya mchezo, kuipatia Nigeria bao la kuongoza.

Lakini wakihamasishwa na mchezaji wao mkongwe nahodha Ahmed Hassan mwenye umri wa miaka 35 , mafarao hao wa Misri walisawazisha bao hilo, kupitia kwa Emad Moteab, kabla ya nahodha huyo Ahmed Hassan na Mohamed Nagui kupachika mengine mawili, na kuwavunja mabawa Tai wa kijani.

Mshambuliaji hatari wa machampion hao watetezi Mohamed Zidan ambaye husukuma kabumbu katika klabu nyingine ya Ujerumani Borrussia Dortmund, alisema kuwa, hawakufikiria kuwa mambo yangekuwa mepesi hivyo kwa wao kupata mabao hayo, na kujipongeza kwa kutokata tamaa baada ya kuwa nyuma kwa bao moja.

Kocha wa Nigeria Shaibu Amodu amekiri kuwa wana kibarua kigumu mbele yao baada ya kipigo hicho ambacho amesema kimetokana na makosa machache waliyofanya ambayo yamewagharimu.

Shaibu aliwapongeza mafarao wa Misri akisema kuwa kiwango chao cha kandanda ni cha hali juu na kwamba washabiki wa soka hiyo jana walishuhudia soka la hali juu kutoka kwa pande zote mbili.

Ama katika pambano lingine,Benin, ilishindwa kuvumilia mashambulizi ya Mamba wa Msumbiji, na kuruhusu kurejeshwa kwa mabao mawili iliyokuwa ikiongoza nayo.

Ulikuwa ni mkwaju wa penalti uliyowekwa wavuni na Razak Omotoyossi, kabla ya beki wa Msumbiji Dario Khan kujifunga mwenye katika dakika 21, vilivyoifanya Benin kuonekana kuondoka na ushindi wa kwanza katika historia yake ya kushiriki  fainali  sita za mataifa ya Afrika.

Lakini Msumbiji ambayo nayo katika historia ya kushiriki kwake katika fainali tatu za michuano hiyo  haijawahi kushinda zaidi ya sare moja, ilisawazisha mabao hayo mawili kupitia kwa Miro na Djidonou.

Leo Simba Wanyika Cameroon watashuka dimbani kuvaana na Gabon, kabla ya Zambia kuingilia na Tunisia

Simba mkongwe Rigobert Song anategemewa hii leo kuweka rekodi ya kucheza fainali ya nane ya Afrika atakapokuwa dimbani kujenga ukuta wa Cameroon.

Rigobert Song  anayeichezea klabu ya Trabzonspor ya Uturuki,tayari ana rekodi ya kucheza mechi zote 33 ambazo Cameroon imecheza katika fainali sita za Afrika tokea alipocheza kwa mara ya kwanza mwaka 1996 nchini Afrika Kusini.

Alikuwa nahodha katika jahazi la Simba hao Wanyika walipounguruma mara mbili mfululizo kutwaa ubingwa huo mwaka  2000 nchini Nigeria na mwaka 2002 nchini Mali.Sasa unahodha amekabidhiwa Simba mwengine mwenye meno makali, Samuel Eto´o

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/IPS

Mhariri: