1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban wajiandaa kwa mashambulio

22 Februari 2007

Kundi la wanamgambo wa Taliban limewaandaa makamanda wake 6000 kwa mapambano dhidi ya serikali na wanajeshi wa kimataifa walioko nchini Afghanistan

https://p.dw.com/p/CHJT
Kikosi cha kimataifa cha ISAF nchini Afghanistan
Kikosi cha kimataifa cha ISAF nchini AfghanistanPicha: AP

Hayo ni kwa mujibu wa kiongozi wa mashambulio wa wanamgambo hao wa kiislamu waliowahi kutawala nchi hiyo.

Kiongozi huyo Mullah Dadullah amesema hayo katika mahojiano na shirika la televisheni la kiarabu Al Jazeera.

Amesema kwamba wanamgambo hao 6000 wa Taliban ama Mujaheedin wako tayari kufanya mashambulio katika kipindi kijacho baada ya msimu wa baridi kali na wamejificha katika mahandaki maalum wakisubiri wakati wa kushambulia.

Dadullah pia amefahamisha pia kuwa idadi ya wapiganaji wa Taliban itaongezeka na kufikia hadi wapiganaji 10,000 hatua ni sawa na kusema kuwa kundi hilo litapata wafuasi zaidi huku nchi wanachama wa mfungamano wa kijeshi wa NATO zikiongezea idadi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan.

Kiongozi huyo amesema namnukuu …Kadiri wanajeshi wa Kikristo na Kiyahudi watakavyo zidi kupambana dhidi yetu ndivyo raia wengi wa Afghanistan watakavyo jiunga nasi..Mwisho wa kumnukuu.

Dadullah mwenye asili ya Kipashtun na anayejulikana kama mpiganaji mkali inaaminika kuwa ni mmoja kati ya washauri wa karibu wa kiongozi wa Taliban Mullah Omar.

Kabla ya mapinduzi dhidi ya utawala wa Taliban yaliyoongozwa na Marekani nchini Afghanistan ya mwaka 2001 Mullah Dadullah alikuwa katika kamati ya watu kumi chini ya uongozi wa Mullah Omar.

Kanali Tom Collins msemaji wa kitengo kinachosaidia maswala ya usalama katika mfungamano wa kijeshi wa NATO – ISAF nchini Afghanistan pia amesema kuwa wapiganaji hao wa Taliban wanajiunda kuzusha mapigano na kwamba vita hivyo vitakuwa vigumu katika maeneo fulani hasa katika maeneo ya kusini ambayo yanadhibitiwa nawapiganaji wa Taliban.

Habari hizo za kujiandaa wapiganaji wa Taliban zimepokewa wakati idadi ya vifo vya maafisa wa ISAF ikiendelea kuongezeka.

Habari za kuuwawa wanajeshi wa kimataifa zimepokelewa kutoka eneo la kusini na mashariki mwa Afghanistan.

Kikosi cha ISAF kikiwa ni pamoja na majeshi yanayoongozwa na Marekani kina wanajeshi elfu 46 nchini Afghanistan.

Katika wiki hii kikosi hicho kiliripoti juu ya kuuwawa kwa mwanajeshi wake mmoja lakini hakuna taarifa zaidi zilizotolewa juu ya kifo chake.

Lakini siku moja kabla serikali za Uhispania na Uingereza zilitangaza kuwa kila moja wapo ilimpoteza mwanajeshi wake mmoja.

Mwanajeshi mwingine wa Uingereza aliuwawa siku ya jumatano baada ya kulipukiwa na bomu lililotegwa ardhini wakati akiwa katika doria katika jimbo la Helmund kusini mwa Afghanistan.

Wanajehsi wengine wawili pia wameuwawa katika mlipuko wa aina hiyo wakati msafara wa kijeshi uliposhambuliwa karibu na mji wa Shindand mashariki mwa Afghanistan.

Wengi kati ya wanajeshi wa kikosi cha ISAF kilicho mashariki mwa Afghanistan ni raia wa Marekani huku eneo la kusini mwa nchi hiyo likiwa zaidi na wanajehsi kutoka Uingereza na Kanada.