1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban wavamia gereza na kuachia wafungwa

14 Septemba 2015

Wanamgambo wa Taliban wamevamia gereza moja katika mkoa wa Ghazni na kuwaachia huru wafungwa zaidi ya 350 mapema hii leo.Tukio hilo limefuatia mashambulizi ya kupangwa na kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1GWLr
Taliban wakiachia huru wafungwa katika gereza hili la Ghazni
Taliban wakiachia huru wafungwa katika gereza hili la GhazniPicha: picture-alliance/dpa/N. Haqjoo

Mapema subuhi ya leo wapiganaji wa kitaliban walivamia gereza la ghazni baada ya kufanya mashambulizi yaliyopangwa kwa ustadi mkubwa ikiwemo kutumia mshambuliaji wa kujitoa muhanga aliyejipenyeza ndani ya gereza hilo kupitia ukuta uliozunguka gereza hilo.Kwa mujibu wa naibu gavana wa mkoa wa Ghazni Mohammed Ali Ahmed wanamgambo wakitaliban walitumia utaalamu wa hali ya juu kufanya zoezi hilo la kuwafungulia wafungwa kiasi 355.

''Watu sita waliovalia magwanda ya jeshi wakiwa na silaha waliingia ndani ya gereza hilo na walichokifanya kwanza kabisa ni kuvunja loki ya lango kuu la kuingia ndani ya gereza na kuanza kuwapigia kelele wafungwa wakiwaambia,sisi ni Taliban tumekuja kuwaachilia huru''alisema Naibu Gavana wa Ghazni

Baada ya tukio hilo inaarifiwa wanamgambo hao wakitaliban waliwaua polisi na kuwaachia huru wafungwa na baadae kuwashambulia wanajeshi waliokimbilia kwenye gereza hilo kwa ajili ya kutoa usaidizi. Tukio hilo limekuja baada ya kufanyika mashambulio kadhaa dhidi ya serikali katika sehemu mbali mbali za nchi hiyo ikiwemo mashambulio mabaya kabisa mjini Kabul yaliyosababisha kutoweka kabisa kwa matumaini ya kufanyika mazungumzo ya amani katika taifa hilo.

Taliban wakiachia huru wafungwa katika gereza hili la Ghazni
Taliban wakiachia huru wafungwa katika gereza hili la GhazniPicha: picture-alliance/dpa/N. Haqjoo

Mwandishi wa habari wa shirika la Reuters amethibitisha kuona maiti mbili za wanaume walioonekana kuwa ni washambuliaji wa kujitoa muhanga zikiwa kando ya gari lililoripuliwa ambalo linasadikiwa ndilo lililotumika kuliripua lango kuu la gereza la ghazni. Aidha Naibu Gavana wa jimbo hilo amesema wapiganaji wanne wa Taliban pamoja na maafisa 7 wa jeshi la serikali wameuwawa kwenye shambulio la leo.n Kwa mujibu wa Naibu huyo Gavana gereza hilo halikuwa na ulinzi mkali kwasababu liko kilomita chache kutoka mjini.Msemaji wa kundi la Taliban Zabihullah Mujahid amedai kupitia barua pepe iliyotumwa kwa vyombo vya habari kwamba wamehusika na tukio hilo.

Naibu Gavana wa Ghazni Mohammed Ali Ahmadi amefahamisha kwamba wafungwa 20 ambao ni hatari kabisa walihamishiwa jela nyingine siku moja kabla ya tukio la leo baada ya kuzuka mapigano ndani ya gereza la Ghazni. Maafisa kaatika mkoa huo wanasema taliban wameshambulia katika kiasi maeneo 10 ya mji huo usiku wa kuamkia leo.Juu ya hilo wizara ya mambo ya ndani imesema wafungwa kiasi 148 miongoni mwa waliotoroka wanatajwa kuwa kitisho kikubwa kwa usalama wa taifa.Hadi sasa mo wafungwa watatu waliokamatwa tena baada ya tukio hilo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Iddi Ssessanga