1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamasha la Beethoven 2010

9 Septemba 2010

Sherehe zinazofanywa kila mwaka, kumkumbuka Ludwig van Beethoven mtungaji wa muziki wa klasik, zinaanza rasmi kesho tarehe 10 Septemba na zitaendelea hadi Oktoba 10, mjini Bonn Ujerumani.

https://p.dw.com/p/P88l
Beethovenfest Bonn 2010 Künstler Quelle: http://www.beethovenfest.de/downloads/1/ Beethoven Orchester
Wanasanii wa Tamasha la Beethoven 2010 mjini Bonn.Picha: Beethovenorchester

"Hadharani - Njozi na Uhuru katika Muziki" ndio kaulimbiu ya tamasha la mwaka huu 2010. Ludwig van Beethoven alikuwa akiwavutia wanamuziki wakati wa enzi yake; na kwa vizazi vya sasa, mwanamuziki huyo ni kipimo chao. Beethoven yungali hai katika ulimwengu wa muziki. Kwa hivyo ni wazi kuwa sherehe za kimataifa za Beethoven katika mji alikozaliwa Bonn, zinahusika na mwanamuziki huyo maarufu.

Mkuu wa tamasha hilo la Beethoven ni Ilona Schmiel. Ni bahati kuwa katika mwaka 1770, Ludwig van Beethoven alizaliwa katika mji wa Bonn. Kwani hivyo,mji huo una umuhimu maalum kote ulimwenguni na itabakia hivyo daima. Schmiel anasema, mji hauwezi kuendelea kuwa maarufu kwa historia yake ya kisiasa tu - kwani kwa kizazi cha sasa, mji mkuu ni Berlin. Kwa mfano, wakati wa safari zake nchini Venezuela, Vietnam au Georgia anachoulizwa ni wapi alikozaliwa Beethoven.

Na sasa katika mji alikozaliwa Beethoven, mara nyingine tena sherehe za muziki zinafikia upeo wake. Zaidi ya burudani na hafla 150 zitafanywa mjini Bonn na ukingoni mwa mji huo. Kama kawaida, sherehe hizo zitakuwa za aina mbali mbali. Ilona Schmiel anafafanua hivi:

" Tamasha kubwa kama hili lazima litafute njia ya kuvutia mashabiki wapya. Kwa mfano kutakuwepo televisheni kubwa kwenye uwanja wa Münsterplatz mjini Bonn. Huko, maelfu ya watu kwa siku tatu mfululizo, wataweza kuona filamu mbali mbali zilizotengenezwa kwa kushirikiana na Deutsche Welle.Hiyo ni njia moja ya kuufikia umma."

Schmiel anasema, njia nyingine ni kupata wasanii watakaojiuliza vipi wangeweza kuwavutia mashabiki zaidi wa kila umri. Kama ilivyo desturi ya Tamasha la Beethoven, umma utaburudishwa na okestra ya vijana iliyo mgeni wa Bonn. Mwaka jana ilikuwa Vietnam. Na mwaka huu, mgeni wa Bonn ni Sinfonica Heliopolis kutoka mji wa Brazil, Sao Paolo. Kushiriki katika tamasha la Beethoven ni muhimu sana kwa okestra hizo za kigeni, kwani ni njia moja ya kubadilishana utamaduni. Schmiel anasema, Beethoven ni maarufu katika nchi nyingi sana na muziki wake unafaa kwa mafunzo ya okestra za vijana.

Mwandishi: Gehrke,Klaus/ZPR

Mhariri:M.Abdul-Rahman