1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yakamata zaidi ya kilo 700 za dawa za kulevya

22 Aprili 2024

Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti dawa za kulevya nchini Tanzania imekamata kilo 767 za dawa za kulevya katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Aprili 4 hadi Aprili 18 mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4f3zD
Cocaine
dawa za kulevya aina ya cocainePicha: Phil Walter/Getty Images

Akizungumza na wanahabari leo, Kamishna Jenerali wa mamlaka ya kupambana na kudhibiti dawa za kulevya, Tanzania, Aretas Lymo, alitoa taarifa ya kukamatwa kwa kilo takribani 767 zadawa za kulevyakatika kipindi cha wiki mbili.

Taarifa ya Kamishna huyo imeeleza kuwa, Mamlaka hiyo imebaini wafanyabiashara wengi wa dawa za kulevya wa Kitanzania, wamekimbilia nchi za nje na wanaendeleza biashara hiyo hapa Tanzania, wakiwa huko kwa kutumia wamiliki wa boti ndogondogo za uvuvi.

dawa za kulevya
dawa za kulevya aina ya heroin zilizokamatwa MsumbijiPicha: Delfim Anacleto/DW

"Moja ya matishio makubwa ya kiusalama duniani ni biashara na matumizi ya dawa za kulevya". 

Mamlaka hiyo imefafanua zaidi kuhusu mbinu mpya za wafanyabiashara hao na kusema, kwa sasa wanafungasha dawa za kulevya katika makopo ya kahawa au chai, ili kuwahadaa maofisa usalama mipakani.

Imeelezwa kuwa, kwa sasa wasambazaji wa dawa za kulevya, wanatumia bandari ndogo zilizorasimishwa na bandari bubu za Dar es Salaam, hususan bandari za Bagamoyo, Kunduchi na  Mbweni, jijini hapa kushusha na kusambaza dawa hizo haramu. Na hapa Kamishna Lymo anatoa onyo.

"Wale wote ambao tutabaini wanahusika kupitisha dawa za kulevya, hata kama ni watumishi  wa serikali, tutahakikisha tunachukua hatua kali."

Hayo yanajiri wakati ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) ya mwaka 2023 ikibainisha kuwa, Afrika imeendelea kuwa eneo la kupitisha dawa za kulevya hasa aina ya cocaine, bangi, na heroin.

Soma pia: Tanzania ni mkondo wa usafirishaji haramu binadamu

Kadhalika UNODC inaeleza kwamba idadi ya watu wanaougua maradhi yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya duniani imepanda kufikia watu milioni 39.5, sawa na ongezeko la asilimia 45 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Tiba ya vitendo kwa waathirika wa dawa za kulevya

Mratibu wa Ajenda ya Vijana kutoka asasi ya bridge for change, Ochek Msuva alikuwa na maoni haya kuhusu mwarobaini wa biashara ya dawa za kulevya nchini na nafasi ya vijana:

"Kuonekana kwa dawa nyingi zikiwa zinaingia mtaani, ni ishara mbaya kwa vijana, baada ya miaka mitatu au mwaka mmoja, tutaona vijana wengi wakiw wameingia kwenye uraibu wa dawa za kulevya, wka hiyo msisitizo wangu naona ni muhimu sanahatua za msingi zikachukuliwa, kwanza kwenye kuwajengea uwezo vijana lakini pili kwenye ku kusaidia dawa zenyewe zisiingie mtaani kwa sababu kuingia mtaani ndio jambo linalotengeneza dawa zisiingie ndani."

Wakati ripoti ya UNODC ikiitaja Afrika kuongoza katika matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi, ripoti zaidi zinaeleza kuwa, asilimia 50 ya matumizi ya dawa za hospitali zinazotumika kama mbadala wa dawa za kulevya, yanafanyika barani Afrika.

Hayo yanajiri wakati dunia ikiwa imebakiza hatua chache tu, kukamilisha malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 yaliyokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, kuhusu kumaliza na kutokomeza biashara ya dawa za kulevya ifikapo 2030.