1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tatizo la udanganyifu katika uchaguzi Afghanistan kupunguzwa

Kabogo Grace Patricia23 Oktoba 2009

Kauli hiyo imetolewa na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Kai Eide

https://p.dw.com/p/KDwn
Kai Eide mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Afghanistan.Picha: AP

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Kai Eide, amesema waandalizi wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini humo wataweza kupunguza lakini sio kumaliza kabisa tatizo la udanganyifu lililotawala katika uchaguzi wa duru ya kwanza.

Kauli hiyo ya Bwana Eide, mwanadiplomasia wa Norway, ameitoa hii leo wakati wa mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO mjini Bratislava, ambapo amesema hatarajii kama ataweza kuondoa tatizo la udanganyifu katika kipindi cha wiki mbili zijazo, ingawa amesema anachotarajia ni kupunguza kwa kiasi fulani udanganyifu huo. Rais aliyeko madarakani, Hamid Karzai wiki hii alikubali kushiriki katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 7 ya mwezi ujao wa Novemba, dhidi ya mpinzani wake mkuu, Abdullah Abdullah, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Afghanistan. Wakati huo huo, Bwana Eide, amesema maafisa wa Afghanistan wameahidi kuwa wasimamizi katika vituo vya kupigia kura ambao walihusika kufanya udanganyifu katika uchaguzi wa mwezi Agosti, watazuiwa kushiriki katika kazi ya aina yoyote ile katika duru ya pili ya uchaguzi.

Idadi ya wasimamizi wa uchaguzi

Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa amesema Tume huru ya Uchaguzi imemuhakikishia kuwa wafanyakazi wote waliohusika moja kwa moja kufanya udanganyifu hawatachaguliwa tena. Amesema maafisa wa Umoja wa Mataifa wataifatilia serikali ili kuhakikisha kuwa wale waliohusika katika udanganyifu hawatafanya kazi katika vituo vya kupigia kura mwezi ujao. Bwana Eide anakadiria kiasi wasimamizi 50,000 hadi 60,000 katika vituo vya kupigia kura watahitajika, chini ya nusu ya wasimamizi 160,000 walichaguliwa kwa ajili ya uchaguzi uliofanyika mwezi Agosti.

Flash-Galerie Wahlen in Afghanistan 2009
Waangalizi wa Kiafghan wakikagua karatasi za kura.Picha: AP

Bwana Eide amesema ana wasi wasi kuhusu watu kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa duru ya pili, kutokana na Wa-Afghan wengi kuhisi kuwa uchaguzi umemalizika na kwamba kampeni ya kuelimisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo ujao, inahitajika. Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi ilikuwa kiasi asilimia 38. Kwa mujibu wa Bwana Eide, waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wanahitajika haraka kwa ajili ya duru ya pili ya uchaguzi na ametoa wito kwa Umoja wa Ulaya kutoa haraka timu ya waangalizi.

Majeshi ya NATO

Kwa upande mwingine, Bwana Eide amesema majeshi yanayoongozwa na NATO nchini Afghanistan yanahitaji majeshi zaidi kutoka mataifa ya Ulaya na haliwezi kuwa suala la Marekani peke yake. Amesema majeshi hayo ni muhimu kwa ajili ya kulinda usalama na kuwapatia mafunzo wanajeshi na polisi wa Afghanistan. Akizungumzia kuhusu suala la wanajeshi nchini Afghanistan, Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen anasema:

''Inagharimu kiasi cha zaidi ya mara 50 zaidi kumgharamia mwanajeshi mmoja tu wa NATO kuliko kumgharamia mwanajeshi wa Afghanistan. Hivyo ina maana kifedha. Pia ina maana kisiasa. Kuwekeza ili kuiwezesha Afghanistan hivi sasa kuna maana kwamba hapo baadaye hutahitaji kuwekeza zaidi.''
NATO Soldaten in Afghanistan
Majeshi ya NATO yakiwa katika shughuli za ulinzi mjini KabulPicha: AP

Kati ya vikosi 100,000 vya kimataifa katika jeshi linaloongozwa na NATO, karibu wanajeshi 68,000 ni Wamarekani. Aidha, amesema anatumai mkutano wa leo wa NATO utaidhinisha mahitaji zaidi ya majeshi ya kimataifa kwa ajili ya kuwapatia mafunzo wanajeshi na polisi wa Afghanistan.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AFP)

Mhariri: M.Abdul-Rahman