1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TBILISI:Uchaguzi wa rais kufanyika mwanzoni mwa Januari

9 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C78i

Kiongozi wa Georgia Mikheil Saakashvili ametangaza kufanyika kwa uchaguzi wa mapema na kuahidi kubatilisha sheria ya hali ya hatari haraka iwezekanavyo.Polisi bado wanaendelea kushika doria mjini Tbilisi kufuatia ghasia kuzuka kati ya majeshi ya usalama na waandamanaji wanaopinga serikali.Bwana Saakashvili anatangaza uchaguzi kufanyika tarehe 5 mwezi Januari.Uchaguzi huo wa rais ulipangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka ujao. Bwana Saakashvili alikabiliwa na shinikizo kutoka jamii ya kimataifa baada ya kutangaza hali ya hatari ya siku 15 baada ya ghasia kutokea siku ya jumatano.Mpaka sasa haijulikani lini hatua hiyo itabatilishwa.Batu Kutelija ni naibu Waziri wa Ulinzi wa Georgia

''Hali ya hatari itabatilishwa haraka iwezekanavyo pale hali itakapokuwa shwari.Tunaiamni kuwa hilo litafanyika katika siku chache zijazo.Hali hiyo ilitangazwa kudumu kwa siku 15 lakini kukiwa shwari itabatilishwa''

Vyama vya upinzani vinakabiliwa na kipindi kigumu cha uchaguzi kwani ni majuma manane pekee yamesali kabla shughuli ya kupiga kura kuanza.Bwana Saakashvili anaungwa mkono na mataifa ya magharibi na anaelezea maandamano ya jumatano kama juhudi za Urusi za kutaka kupindua serikali.

Georgia inatangaza kuwafukuza wanadiplomasia watatu wa Urusi kwa madai ya kuhusika na ujasusi hatua ambayo Urusi imelipiza kwa kuwafukuzawanadiplomasia wa Georgia kutoka mjini Moscow. Umoja wa kujihami wa mataifa ya Ulaya NATO unashtumu ghasia hizo vilevile hatua ya kutangaza hali ya hatari.Umoja huo aidha umeidhinisha Georgia kuwa katika orodha ya wanachama wapya jambo linaloghadhabisha Urusi.