1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Teddy Bear yazusha mzozo wa kisiasa kati ya Sudan na Uingereza

Maja Dreyer29 Novemba 2007

Kesi ya mwalimu wa asili ya Kiingereza aliyepelekwa mbele ya mahakama mjini Khartoum leo, imezusha mzozo kati ya serikali za Uingereza na Sudan. Cha kuanzisha mzozo huu ni mtoto wa sanamu mwenye umbo la dubu, Teddy Bear.

https://p.dw.com/p/CUkB
Teddy BearPicha: AP

Dali huyo au mtoto wa sanamu aina ya Teddy Bear ulipelekwa shuleni na mmoja ya wanafunzi wa mwalimu huyu Bibi Gillian Gibbons anayetokea Liverpool, Uingereza na alikwenda Khartoum kufundisha kwenye shule ya kibinafsi. Bi Gillions aliwauliza watoto wanataka kumwita jina gani doli huyo mwenye umbo la dubu. Mmoja alipendekeza jina lake mwenyewe, Mohammed, na wengine walikubali pamoja na mwalimu.


Leo hii, mwalimu huyu Bi Gibbons alipelekwa mbele ya mahakama ya mjini Khartoum akishtakiwa kuutusi Uislamu kwa sababu hakuzuia watoto kumwita Teddy Bear jina la mtume Mohammed. Pia anashtakiwa kusababisha chuki na kudharau dini. Ikiwa mahakama itamtia hatiani, Bibi huyu anaweza kucharazwa viboko arubaini, kutoa faini au kufungwa gerezani kwa muda wa miezi kadhaa.


Huko Uingereza, waziri wa masuala ya nje, David Miliband alisema kesi hiyo ni kosa lililofanywa bila ya kujua vizuri zaidi. Pia waziri mkuu Gordon Brown alitaja wasiwasi zake kuhusu mwalimu huyu wa Uingereza: “Nimesikitishwa sana na yaliyomtokea Gillian Gibbons. Naweza kuthibitisha kwamba ubalozi wetu mjini Khartoum unamsaidia kwa kila iwezalo.”


Balozi wa Sudan nchini Uingereza Khalid al Mubarak aliyeitwa na serikali huko London kuelezea matokeo ya Khartoum alisema utaratibu wa kisheria unaoendelea ni wa haki: “Sisi tuna mfumo wa sheria, na mfumo huu unahakikisha haki za mtuhumiwa au mshtakiwa. Kesi hiyo inaweza kuelekea upande tofauti, maana yake jaji anaweza kuamua kufuta kesi na kumwachia huru.”


Waziri Miliband wa Uingereza alisema mfumo wa kisheria wa Sudan unatambuliwa hata hivyo nchi yake inaomba katika kesi hiyo wahusika watoe uamuzi wa busara. Iwapo kesi haitatatuliwa haraka, kundi la wabunge wa Uingereza wanataka kumshawishi rais wa Sudan Omar al-Bashir kumwachia huru Bi Gillian Gibbons. Pia jumuiya ya Waislamu wa Uingereza wanataka, mwalimu huyu aachiliwe huru.


Bi Gillian Gibbons alikamatwa Jumapili iliyopita baada ya wazazi wa wanafunzi wake walimlaumu kutowazuia watoto waliompa doli huyo jina la mtume Mohammed. Mwalimu huyu aliyetembelewa na wajumbe wa ubalozi wa Uingereza anasema anatendwa vizuri lakini hakutaka kumtusi yeyote kwa kumwita Teddy jina hilo.