1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN : Ahmedinejad ataka kuhudhuria Baraza la Usalama

11 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKC

Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran angelipendelea kuhudhuria mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutetea mpango wa nuklea wa Iran.

Televisheni ya taifa nchini Iran imemkariri msemaji wa serikali ya Iran Gholam Hossein Elham akisema kwamba rais wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran anakusudia kuhudhuria mkutano wa Baraza la Usalama utakaojadili suala la nuklea la Iran ili kutetea haki ya taifa la Iran katika kutumia nishati ya nuklea kwa dhamira za amani.

Repoti hiyo haikufafanuwa wakati gani Ahmedinejad anapanga kuhudhuria mkutano huo na iwapo amealikwa na Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Repoti hiyo katika televisheni ya taifa ya Iran inakuja siku chache baada ya shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomu kusitisha takriban miradi 24 ya misaada ya nuklea kwa Iran katika hatua ambayo yumkini ikaathiri ushirikiano wa Iran na chombo hicho cha Umoja wa Mataifa kinachosimamia masuala ya nuklea duniani.