1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN: Iran kujiunga na mpango wa Venezuela na Cuba

2 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBmi

Iran inapanga kujiunga na mpango wa Amerika Kusini unaolenga kukabiliana na juhudi za Marekani kutaka biashara huru katika eneo hilo. Rais wa Venezuela, Hugo Chavez, akiwa katika ziara ya siku mbili nchini Iran ameukaribisha uanachama wa Iran katika mpango huo unaoungwa mkono na Venezuela na Cuba.

Rais Hugo Chavez na Fidel Castro wa Cuba walisaini mpango huo mnamo mwaka wa 2005 kuzikosoa juhudi za Marekani kupanua biashara huru na nchi za Amerika Kusini. Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, amesema nguzo za ukaidi wa kimataifa zimekuwa zikitikisika na ushindi utapatikana kwa kuendeleza upinzani na kuwa imara.

Rais Hugo Chavez kwa upande wake amesema ushirikiano kati ya nchi huru kama vile Iran na Venezuela unaweza kuwa na jukumu muhimu katika kuzishinda sera za kibeberu.