1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN: Rais Ahmadinejad asema nchi yake haitabanduka

16 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCIP

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, amesema leo kwamba azimio jipya la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa halitaubadili msimamo wa Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Rais Ahmadinejad ameyasema hayo siku moja baada ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani kukubaliana juu ya azimio jipya linaloviongezea ukali vikwazo dhidi ya serikali ya Tehran kwa kupuuza masharti ya kusitisha urutubishaji wa madini ya uranium.

Rais Mahmoud Ahmadinejad, amelaani vikwazo hivyo vipya vya Umoja wa Mataifa na ametuma ombi rasmi kwa umoja huo aruhusiwe kulihutubia mwenyewe baraza la usalama. Matamshi ya rais Ahmadinejad yamemuudhi balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Alejandro Daniel Wolf.

´Naona ni kejeli kwamba rais Ahmedinejad ambaye amenukuliwa leo akisema huyachana maazimio ya baraza la usalama na haheshimu kazi yake, anataka kuja kuzungumza na baraza hilo.´

Azimio jipya dhidi ya Iran limewasilishwa kwa wanachama wote 15 wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ili wajiandae kulipigia kura wiki ijayo.