1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN:Waziri Mkuu wa Iraq awasili Iran kutafuta amani ya nchi yake

8 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBb0

Waziri Mkuu wa Iraq, Nour al Maliki amewasili nchini Iran kwa ajili ya mazungumzo na maafisa wa nchi hiyo yenye nia ya kutafuta suluhisho la kiusalama nchini mwake.

Iran imekuwa ikishutumiwa na Marekani kuwa inachangia hali mbaya ya usalama nchini Iraq kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa kishia.

Ziara hiyo ya Nour al Maliki inakuja siku chache tu baada ya wanadiplomasia wa Iran na Marekani kuwa na mazungumzo mjini Baghdad yenye kulenga kutafuta amani nchini Iraq.

Aidha ziara hiyo inakuja mnamo wakati ambapo serikali ya Waziri Mkuu huyo wa Iraq inakabiliwa na shinikizo kubwa la ndani na nje.

Iran na Iraq zilipigana vita ya miaka minane katika miaka ya 80, lakini uhusiano kati ya jamii ya washia wa Iran na wale wa Iraq wanaounda sehemu kubwa ya serikali ya Iraq umekuwa ukiongezeka.

Waziri Mkuu Nour al Maliki alilakiwa kwenye uwanja wa ndege na Makamu wa Rais wa Iran Parviz Davood na alitarajiwa kuwa na mazungumzo na kiongozi wa kiroho wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, Rais Mahmoud Ahmednejad pamoja na katibu mkuu wa baraza la usalama la Iran Ali Larijan.

Akiwa njiani Waziri Mkuu wa Iraq aliwaambia waandishi wa habari ya kwamba anatarajia ziara hiyo itafungua ushirikiano mpya katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kiulinzi kati ya nchi hizo mbili.

Amesema kuwa anataraji kutiliana saini makubaliano katika maeneo kadhaa na nchi hiyo.

Waziri huyo Mkuu wa Iraq anatokea Uturuki ambako alikuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan.

Katika ziara hiyo viongozi hao walikubaliana kushirikiana katika kukisambaritisha kikundi kilichojitenga cha wakurdi huko kaskazini mwa Iraq.

Uturuki kwa muda mrefu imekuwa ikiitaka Iraq kuwasambaratisha wanachama wa kikundi cha PKK ambacho kinachokuliwa kama cha kigaidi.