1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko la ardhi laua Uturuki

Abdu Said Mtullya25 Oktoba 2011

Waokoaji nchi Uturuki wanaendelea na juhudi za kuwatafuta watu waliokwama kwenye vifusi vya majengo baada ya tetemeko kubwa la ardhi kupiga mji wa mashariki mwa nchi hiyo, Van, hapo jana na kuua zaidi ya watu 200.

https://p.dw.com/p/12y92
Tetemeko kubwa la ardhi laipiga Uturuki.
Tetemeko kubwa la ardhi laipiga Uturuki.Picha: AP

Mpaka sasa watu wasiopungua 275 wamekufa kutokana na tetemeko hilo lililoikumba sehemu ya mashariki mwa Uturuki ambako watu wamelazimika kulala nje kwa siku ya pili katika baridi kali. Waokoaji wanaotumia taa zinazotumia nguvu za majenereta na zana zingine nzito, wameendelea kuwatafuta walionusurika katika mji wa Ercis uliokumbwa vibaya sana na maafa ya tetemeko.

Huduma za maji na umeme zimekatika katika mji huo kutokana na tetemeko. Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alieutembelea mji wa Van, ambako tetemeko la ardhi lilianzia amesema takriban nyumba zote zilizojengwa kwa matofali ya udongo zimesambaratika katika vijiji vinavyouzunguka mji huo. Taarifa zaidi zinasema mitetemeko mingine zaidi ya 200 ilifuatia.