1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Thatcher aaga dunia

9 Aprili 2013

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Margaret Thatcher, maarufu kama "Iron Lady" kutokana na ujasiri na ukakamavu wake katika medani za uongozi, amefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kiharusi akiwa na miaka 87.

https://p.dw.com/p/18Bov
Margaret Thatcher
Margaret ThatcherPicha: William Lovelace/Express/Getty Images

Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza na Waziri Mkuu David Cameron wameongoza katika salamu za rambi rambi kwa waziri mkuu huyo wa kwanza mwanamke nchini Uingereza, muumini mashuhuri kabisa wa sera za mrengo wa kulia na mtu muhimu wakati wa Vita Baridi.

Msemaji wa familia ya Thatcher amekaririwa akisema "kwa masikitiko makubwa Mark na Carol Thatcher (watoto wa marehemu) wanatangaza kwamba mama yao Bi. Thatcher amefariki kwa utulivu baada ya kupigwa na kiharusi leo asubuhi."

Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye aliiongoza Uingereza kuanzia mwaka 1979 hadi mwaka 1990 alikuwa akikabiliwa na maradhi ya kupoteza kumbukumbu na mara chache amekuwa akionekana hadharani katika miaka ya hivi karibuni.

Thatcher alikatazwa kuhutubia hadharani

Waziri Mkuu wa zamani nchini Uingereza Margaret Thatcher.
Waziri Mkuu wa zamani nchini Uingereza Margaret Thatcher.Picha: picture-alliance/dpa

Mara ya mwisho alilazwa hospitalini hapo mwezi wa Disemba mwaka jana kwa ajili ya operesheni ndogo ya kuondowa uvimbe kwenye nyonga yake.Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha Conservative amebakia kuwa waziri mkuu pekee mwanamke katika historia ya Uingereza na kiongozi aliekaa mfululizo kwa muda mrefu kabisa katika makaazi ya waziri mkuu ya Downing Street katika karne ya 20.

Binti yake wakati fulani aliwahi kusema kwamba waziri mkuu huyo wa zamani inabidi akumbushwe mara kwa mara kwamba mume wake Denis amefariki mwaka 2003.Thatcher alitakiwa na madaktari kuacha kuhutubia hadharani muongo mmoja uliopita baada ya kukumbwa na kiharusi mara kadhaa.

Kasri la Kifalme la Uingereza Buckingham Palace limetowa taarifa ikisema kwamba Malkia amesikitishwa kusikia habari za kifo cha Thatcher na kwamba atatuma ujumbe binafsi wa masikitiko kwa familia.Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amekatisha ziara yake katika nchi kadhaa za Ulaya na amesema kwamba kwa huzuni kubwa amepokea habari za kifo cha Bibie huyo na kwamba wamempoteza kiongozi adhimu,waziri mkuu adhimu na Muingereza adhimu.

Thatcher aiokowa Uingereza

Waziri Mkuu wa zamani Margaret Thatcher akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa sasa David Cameron hapo mwaka 2010.
Waziri Mkuu wa zamani Margaret Thatcher akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa sasa David Cameron hapo mwaka 2010.Picha: Leon Neal/AFP/Getty Images

Ameongeza kusema kwamba Thatcher "ameitumikia nchi yake vizuri sana, ameiokoa nchi yake na ameonyesha ushujaa mkubwa sana katika kufanya hivyo.Watu watakuwa wanajifunza juu ya kile alichokifanya na mafanikio yake kwa miongo kadhaa inayokuja na yumkini hata kwa karne kadhaa.Hiyo dio haiba yake."

Michael Howard kiongozi wa chama cha Conservative kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2005 amekiambia kituo cha televisheni cha Sky kwamba ni habari za kuhuzunisha sana kwani alikuwa ni mashuhuri sana katika siasa za Uingereza.Howard anaamini kwamba Thatcher ameiokoa nchi yao, ameubadili uchumi wa nchi hiyo na anaamini kwamba ataingia katika historia akiwa kama mmojwapo wa mawaziri wao wakuu walio adhimu kabisa.

Wafuasi wa sera za mrengo wa kulia wanampongeza mama huyo kwa kuitowa Uingereza kwenye msononeko wa kiuchumi lakini wafuasi wa mrengo wa shoto wanamshutumu kwa kuving'owa viwanda vilivyokuwepo tokea enzi za jadi na kuvunja kiini cha mshikamano wa jamii.

Alielewana vyema na Reagan

Waziri Mkuu Margaret Thatcher akifurahia jambo na Rais Ronald Reagan wa Marekani katika Mkutano wa Kilele wa Ottawa mwaka 1981
Waziri Mkuu Margaret Thatcher akifurahia jambo na Rais Ronald Reagan wa Marekani katika Mkutano wa Kilele wa Ottawa mwaka 1981Picha: picture alliance/AP Images

Katika jukwaa la kimataifa alijenga uhusiano maalum na Rais Ronald Reagan wa Marekani jambo ambalo limesaidia kuuangusha ukomunisti katika Muungano wa Kisovieti.Alimwelezea aliekuwa kiongozi wa Muungano wa Kisovieti wakati huo Mikhail Gorbachov kuwa ni mtu anayeweza kushirikiana naye.Pia alikuwa akipinga vikali uhusiano wa karibu wa Ulaya.

Thatcher alizaliwa akiwa anajulikana kwa jina la Margaret Hilda Roberts hapo tarehe 13 Oktoba mwaka 1925 katika mji wa soko wa Grantham mashariki ya Uingereza akiwa ni binti wa muuza duka la vyakula na bidhaa ndogo ndogo.Baada ya kumaliza shule na kujipatia shahada yake ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Oxford alifunga ndoa na mfanyabiashara Denis hapo mwaka 1951 na miaka miwili baade walibarikiwa watoto mapacha Carol na Mark.

Mara ya kwanza alichaguliwa katika bunge hapo mwaka 1959 na alichukuwa nafasi ya waziri mkuu wa zamani Edward Heath kama kiongozi wa chama cha upinzani cha Conservative hapo mwaka 1975 kabla ya kuwa waziri mkuu miaka minne baadae.

Haiba aliyoiwacha

Vikosi vya Argentina vilipovamia visiwa vya Falklands mwaka 1982.
Vikosi vya Argentina vilipovamia visiwa vya Falklands mwaka 1982.Picha: picture-alliance/dpa

Haiba yake ya kudumu inaweza kuelezwa kwa muhtasari kuwa ya "Thatcherism " yaani mkusanyiko wa sera ambapo wafuasi wake wanasema zimeendeleza uhuru wa mtu binafsi na kusambaratisha mgawanyiko wa kitabaka ambao ulikuwa umeipasuwa Uingereza kwa karne kadhaa.Hata hivyo kushinikiza sera zake kuliiweka serikali yake katika mapambano kadhaa magumu ndani na nje ya nchi.

Alipambana na migomo ya mara kwa mara ya vyama vya wafanyakazi ambapo alifanikiwa kuzima nguvu za vyama hivyo na kuondowa ruzuku kwa makampuni kadhaa yaliokuwa yakiendeshwa kwa hasara.Itakumbukwa wakati Argentina ilipovivamia visiwa vya Falklands vilivyoko chini ya himaya ya Uingereza hapo mwaka 1982, Thatcher alituma vikosi na meli za kivita na kuvikombowa katika kipindi cha miezi miwili.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef