1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theluji yaendelea kukwamisha safari za ndege barani Ulaya

21 Desemba 2010

Theluji imeendelea kutatiza usafiri barani Ulaya, huku uwanja wa ndege wa Frankfurt hapa Ujerumani ukisitisha safari za ndege tena hii leo, kutokana na theluji nyingi iliyoanguka

https://p.dw.com/p/QhHj
Theluji yakwamisha ndege FrankfurtPicha: picture-alliance / dpa

Safari za ndege katika uwanja wa Frankfurt hapa Ujeumani zimecheleweshwa tena hii leo kutokana na theluji nyingi iliyoanguka. Ndege moja tu imeruhisiwa kutua katika uwanja huo mapema leo mwendo wa saa 8:28.

Wakati huo huo, wafanyakazi wawili wa reli wameuwawa usiku wa kuamkia leo wakati treni ilipowagonga wafanyakazi wa timu ya kufanya ukarabati, walipokuwa wakiondoa theluji kwenye reli, kati ya mji wa Cologne na Mulheim. Msemaji wa shirika lisafiri wa treni hapa Ujerumani, Deutsche Bahn, amesema safari za leo zitacheleweshwa na nyengine kufutwa kabisa kutokana na kuendelea kuanguka kwa theluji nyingi.

Hali hiyo ya hewa imesababisha matatizo makubwa katika barabara za maeneo kadhaa ya magharibi mwa Ujerumani, huku polisi katika sehemu kadhaa za nchi wakisema hali imeanza kuwa nzuri na kwamba ajali chache za barabarani zimetokea katika siku zilizopita.

Nchini Uingereza theluji na viwango vya chini vya joto vimeendelea kukwamisha safari za ndege kuingia na kutoka nchini humo hii leo, huku abiria waliokuwa na matumaini ya kuwahi sherehe za sikukuu ya Krismasi wakikabiliwa siku nyengine ya kucheleweshwa kwa safari zao na hata kufutwa kwa siku kadhaa.

Shirika la ndege la Uingereza, British Airways, linatarajiwa kufuta idadi kubwa ya safari zake kutoka uwanja wa ndege wa Heathrow jijini London, ambao unatarajiwa kufungua moja kati ya njia zake mbili za ndege hii leo. Maelfu ya abiria wamekwama katika uwanja wa Heathrow kwa siku kadhaa sasa kufuatia safari zao kucheleweshwa au kufutwa.

Nchini Ufaransa, maafisa wameendelea na jitihada za kuondoa orodha ndefu ya safari za ndege zilizocheleweshwa na kuwaangalia abiria ambao wangali wamekwama leo kutokana na theluji nyingi. Naibu waziri wa usafiri wa Ufaransa, Thiery Mariani, amesema uwanja mkubwa wa ndege mjini Paris, ambako watu 3,000 wamelala usiku wa kuamkia leo, umeanza kufanya kazi, ili kuwasafirisha abiria waliokwama kwa muda mrefu.

Shirika la ndege la Ufaransa, Air France, limesema leo kwamba hali ya hewa ya msimu huu baridi italigharimu Euro kati ya milioni 25 na milioni 35.

Mwandishi: Josephat Charo/DPAE/APE/RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman