1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theluji yatatiza usafiri barani Ulaya

20 Desemba 2010

Theluji nyingi imetatiza usafiri wa abiria wanaojaribu kuwahi kufika nyumbani kwa ajili ya sikukuu ya Krismasi barani Ulaya, na kulazimu viwanja vikubwa vya ndege kufungwa. Safari 300 za ndege zimefutwa leo Frankfurt

https://p.dw.com/p/QgJ7
Mamia ya abiria waliokwama katika uwanja wa FrankfurtPicha: AP

Maafisa katika uwanja wa ndege wa Frankfurt wamefuta safari 300 za ndege mapema leo (20.12.2010) huku theluji zaidi ikitarajiwa kuanguka, siku moja tu baada ya mamia ya safari nyengine kufutwa. Msemaji wa uwanja huo amesema njia za ndege ziko wazi na theluji haianguki kwa sasa, lakini wanatarajia kiwango cha hadi sentimita tatu za theluji kuanguka wakati wa mchana.

Hapo jana zaidi ya safari 540 za ndege zilifutwa kutokana na theluji nyingi na kwa kuwa viwanja vingine vya ndege barani Ulaya vilikuwa vimefungwa. Mamia ya abiria walilazimika kulala katika uwanja wa ndege wa Frankfurt katika mazingira magumu, huku kumbi za uwanja huo zikijaa pomoni abiria.

Abiria wengi walivunjika moyo kwa kushindwa kusafiri, hali iliyowafanya kujawa na ghadhabu. "Nimekasirika sana. Kila niliyemuuliza, hata wafanyakazi wa Lufthansa, hawana habari wala bazi. Mmoja wao hana kompyuta, mwengine hana taarifa, mwingine anagawa tu vyakula vitamu. Ni hali ya kutisha," amesema abiria mmoja.

Na kwa wale wanaojaribu kufika nyumbani kusherehekea sikukuu ya Krismasi, matumaini ya kujumuika na jamaa zao polepole yanadidimia. Abiria mmoja amesema, "Inavunja moyo kwa kweli wakati huu, nikijaribu kufika nyumbani kwa ajili ya sikukuu ya Krismasi."

Winterchaos
Abiria waliokwama katika uwanja wa Heathrow jijini LondonPicha: picture alliance / empics

Kampuni ya safari za reli ya Ujerumani, Deutsche Bahn, imesema safari ndefu za treni zitacheleweshwa leo kutokana na hali hiyo ya hewa.

Nchini Uingereza, ndege chache zimepaa na kushuka katika uwanja wa ndege wa Heathrow mjini London mapema leo, baada ya uwanja huo kufungwa mwishoni mwa juma kwa sababu ya theluji na barafu. Abiria wengi wamekwama kwa siku ya tatu hii leo huku safari zikicheleweshwa na kufutwa katika uwanja huo.

Andrew Teacher wa kampuni inayosimama uwanja wa Heathrow, BAA amesema, "Tutafanya kazi bila kupumzika katika saa chache zijazo, na katika siku zijazo, kukabiliana na matatizo yanayosababishwa na hali hii ya hewa. Jambo moja tulilojifunza ni kwamba hatuwezi kubashiri kitakachotokea. Tunachoweza kukifanya kwa uwezo wetu wote ni kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wetu pamoja na abiria hapa katika uwanja wa Heathrow."

Schnee auf Flughafen Frankfurt am Main
Ndege ya shirika la Lufthansa ikiwa imekwama katika uwanja wa ndege wa FrankfurtPicha: AP

Nchini Uholanzi, mamia ya abiria walilala katika uwanja wa ndege wa Schipol mjini Amsterdam ambako safari za ndege zilitatizwa hapo jana. Nchini Ubelgiji watu takriban 1,500 walilala katika uwanja wa ndege wa Brussels kwa siku ya pili, wengi wao wakiwa katika safari za ndege 18 zilizokuwa zipitie uwanja wa Heathrow jijini London. Mtu mmoja alikufa katika eneo la Ubelgiji la Wallonia wakati paa la nyumba lilipomuangukia kutokana na theluji nyingi.

Kaskazini mwa Italia hali imeanza kuwa nzuri kufuatia siku mbili za matatizo ya usafiri wa barabarani na katika viwanja vya ndege huko Tuscany. Katika eneo la Balkan, watu wanne walikufa kutokana na baridi kali mwishoni mwa juma. Wanaume wawili wenye umri wa miaka 72 na 50, walipatikana wamekufa karibu na Banja Luka huko Bosnia, huku wengine wawili wakapatikana na majira zao huko Serbia.

Huko Ufaransa, safari tatu kati ya kumi za ndege zimefutwa leo katika uwanja mkubwa wa ndege mjini Paris. Wakati huo huo, abiria watatu wameuwawa baada ya treni moja kuigonga motokaa kaskazini mwa nchi hiyo.

Ajali hiyo imetokea wakati theluji nyingi ikiendelea kuvuruga usafiri katika eneo hilo, lakini maafisa wa timu ya uokozi hawakuweza kuthibitisha mara moja kama kama ajali hiyo imesababishwa na hali hiyo ya hewa. Abiria wote watatu walikuwa ndani ya motokaa hiyo wakati ilipogongwa katika kivuko cha Maubeuge, karibu na mpaka na Ubelgiji, lakini hakuna abiria aliyejeruhiwa katika treni hiyo.

Mwandishi: Josephat Charo/DPAE/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman