1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tillerson anazuru Uturuki

Grace Kabogo
30 Machi 2017

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson amewasili mjini Ankara, Uturuki ambapo kwa sasa anakutana na viongozi wa Uturuki.

https://p.dw.com/p/2aJGk
Rex Tillerson Anti -IS- Koalition Washington
Picha: picture alliance/dpa/C. Owen

Ziara hiyo inafanyika siku moja baada ya Uturuki kusema imekamilisha operesheni zake za kijeshi kaskazini mwa Syria, huku kukiwa na tofauti kati yake na Marekani kuhusu jinsi ya kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Tillerson anakutana na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, Waziri Mkuu, Binali Yildirim pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Mevlut Cavusoglu.

Tillerson ni afisa wa ngazi ya juu kabisa wa Marekani kuzuru Uturuki, tangu Rais Donald Trump alipoingia madarakani, Januari 20 mwaka huu. Ziara hiyo inaonekana kama juhudi za kujaribu kuimarisha uhusiano kati ya Uturuki na serikali mpya ya Marekani.

Maafisa kutoka nchi hizo mbili ambazo ni washirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, wamesema miongoni mwa masuala yatakayozungumzwa na viongozi hao ni pamoja na mzozo wa Syria ambao sasa umedumu kwa miaka sita. Uhusiano kati ya Uturuki na Marekani ulizorota wakati wa utawala wa Barack Obama kutokana na hatua ya Marekani kushirikiana na wanamgambo wa Kikurdi wa Syria, wanaopambana na kundi la IS nchini Syria.

Gulen na afisa wa Halkbank pia kujadiliwa

Masuala mengine ambayo huenda yakajadiliwa ni pamoja na maombi ya Uturuki kuhusu kurejeshwa nyumbani kiongozi wa kidini anayeishi nchini Marekani, Fethullah Gulen, anayeshutumiwa kwa kupanga jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwaka uliopita, ingawa amekanusha madai hayo. Pia Uturuki italigusia suala la kukamatwa mjini New York, kwa afisa mtendaji wa benki ya Uturuki ya Halkbank. Afisa huyo anatuhumiwa kwa kuisaidia Iran kukiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Türkei Istanbul  Refenrendum Werbebanner Erdogan
Bango linaloonyesha picha ya Rais ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/E. Gurel

Ziara ya Tillerson inafanyika chini ya wiki tatu kabla ya kura ya maoni ambayo inatafuta kuifanyia katiba ya Uturuki marekebisho ili kuweza kumuongezea mamlaka zaidi Rais Erdogan, hatua ambayo wapinzani wake na baadhi ya washirika wa Ulaya wanahofia itaongeza utawala wa kimabavu.

Maafisa waandamizi wa Marekani wamesema hata hivyo Tillerson hatokutana na wanachama wa upinzani wakati wa ziara yake hiyo, ishara inayoonyesha kwamba anatafuta kuepukana na hatua ya kuingilia masuala ya ndani ya Uturuki, wakati akijaribu kuangazia zaidi mapambano dhidi ya kundi la IS.

Hayo yanajiri wakati ambapo Uturuki imesema imekamilisha operesheni zake za kijeshi kaskazini mwa Syria, ingawa hajatoa maelezo zaidi iwapo hiyo ni ishara ya kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Syria au la. Jana usiku Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildrim alisema kwamba operesheni hiyo imekamilika baada ya majeshi yake na waasi ambao ni washirika wao kuyakomboa maeneo yaliyoko katika mpaka wa Uturuki na Syria.

''Kila kitu kimedhibitiwa na maisha yamerejea kama kawaida na iwapo kuna haja ya kuendelea na mapambano, basi operesheni mpya itatangazwa na kupewa jina jipya, alisema Yildrim.'' Jeshi la Uturuki na waasi washirika wao wa Syria, walianzisha operesheni hizo mwezi Agosti mwaka uliopita, wakiwalenga wanamgambo wa kundi la IS na wanamgambo wa Kikurdi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, AP, AFP
Mhariri: Saumu Yusuf