1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timor ya Mashariki huenda ikapata serekali ya mseto

6 Julai 2007

Timor ya Mashariki leo inaonekana inajitayarisha kuwa na serekali ya mseto itakayoongozwa na kiongozi wa mapambano ya uhuru, Xanana Gusmao, baada ya wiki iliopita kufanyika uchaguzi wa bunge katika nchi hiyo ilio katika matatizo.

https://p.dw.com/p/CHBP
Xanana Gusmao, anayetarajiwa kuwa waziri mkuu mpya wa Timor ya Mashariki.
Xanana Gusmao, anayetarajiwa kuwa waziri mkuu mpya wa Timor ya Mashariki.Picha: AP

Chama cha Gusmao kimeunda muungano na makundi madogo madogo ili kufikia wingi unaohitajiwa ili kulitawala taifa hilo lililo maskini.

Pindi muungano huo utakubaliwa, basi utafungua ukurasa mpya katika historia ya michafuko ya taifa hilo changa na kukiwacha chama tawala cha zamani, FRETILIN, katika upinzani, licha ya kwamba kimepata sehemu kubwa ya kura zilizopigwa.

Chama cha National Congress and Reconstruction cha Xanana Gusmao, CNRT, kitashirikiana na Chama cha Social Democratic na kile cha Democratic. Kwa pamoja vyama hivyo vimepata asilimia 51 ya kura. Chama cha CNRT, kilichoundwa mwanzoni mwa mwaka huu, kilipata asilimia 24 ya kura. Katika taarifa, vyama hivyo vilisema vinataraji muungano huo utaweza kuhakikisha wingi ulio wenye nguvu na wa kudumu. Vilisema mseto huo utakuwa na wingi bungeni, umeuitikia mwito wa kuunda serekali, na kwamba maelezo zaidi juu ya makubaliano hayo yataamuliwa baadae na kuwasilishwa kwa wananchi. Lakini Chama cha FRETILIN kilisema hakijakubali kuketi upande wa upinzani, kikiashiria kwamba kutakuweko malumbano ya kisheria hapo baadae. Chama hicho kilichotamba katika siasa za Timor ya Mashariki tangu kilipowekwa madarakani mwaka 2001, kilipata asilimia 29 ya kura zilizopigwa na kuwaniwa na vyama 14. Lakini huo haujawa wingi wa kutosha kuweza kuunda serekali kutoka bunge la viti 65. Mshauri wa cheo cha juu wa Chama cha FRETILIN, Harold Moucho, alisema haukatai uwezekano wa wao kuunda serekali yao wenyewe au uwezekano wa kuunda serekali na vyama vingine. Alisema mtu hawezi kukiweka pembeni chama kilichopata kura nyingi.

Apolinario Mendes de Carvalho, mkuu wa wawasimamizi wa uchaguzi huo kutoka Jumuiya ya Nchi zinazozozungumza lugha ya Kireno, alisema:

+Tunatoa mwito kwa jamii ya kimataifa itoe msaada kwa Timor ya Mashariki katika hatua hii muhuimu ya kuendelea kujenga na kuimarisha taasisi zake…+

Mahakama ya Rufaa ya Timor ya Mashariki lazima ihakikishe juu ya matokeo hayo ya uchaguzi na baadae mseto huo upewe kibali cha kuunda serekali na Rais Ramos-Horta. Rais huyo alisema ni yeye atakayeamua kutokana na moyo na maneno yaliomo ndani ya katiba vipi kati ya vyama mbali mbali vitakavoweza kumshawishi kihalali kwamba vinaweza kuunda serekali itakayokuwa imara na ya kudumu. Inatarajiwa kwamba Rais Ramos-Horta atakiomba kwanza chama cha FRETILIN kiunde serekali, na ikiwa kitashindwa basi chama cha CNRT kitaombwa. Bila ya kujali nani atakaekamata madaraka, chama kitakachhotawala huenda kikawa na shida ya kupitisha bajeti bungeni pindi wabunge watabadilisha upande, jambo litakalolazimisha kufanywe uchaguzi mpya.

Serekali mpya itakabiliwa na na kazi kubwa kwa vile Timor ya Masharikiu inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na matatizo ya kijamii.

Uchaguzi huu wa bunge uliitishwa kutokana na michafuko na mivutano ya kisiasa tangu yalipotokea mapigano katika mabarabara ya mji mkuu wa Dili mwezi April na May mwaka jana. Michafuko hiyo ilichukuwa roho za si chini ya watu 37 na kuwalazimisha watu 150,000 kuwekwa makambini. Wanajeshi wa kimataifa wa kuweka amani pamoja na polisi 1,700 wa kutoka Umoja wa Mataifa wamerejesha utulivu. Bado wako katika hali ya tahadhari. Chama cha FRETILIN kimepoteza kura na kimeadhibiwa kwa kushindwa kuzuwia michafuko ya mwaka jana na kuikwamua nchi hiyo kutoka kwenye umaskini. Licha ya kwamba kuwa na utajiri wa hifadhi za mafuta na gesi ya ardhini, ukosefu wa kazi katika Timor ya Mashariki unakaribia asilimia 50. Nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 2002 baada ya kuweko mapigano makali ya kujitenga kutoka Indonesia miaka mitatu kabla. Iliwahi kutawaliwa na Ureno kwa zaidi ya karne nne.