1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu kujikatia tikiti za awamu ya mtoano

4 Novemba 2014

Timu tatu ambazo zimeendelea kutamba katika Champions League msimu huu zinaweza kukata tikiti zao katika awamu ya mtoano kukiwa bado michezo miwili katika awamu ya makundi

https://p.dw.com/p/1DgiK
Bayer 04 Leverkusen Training
Picha: picture-alliance/dpa/F. Gambarini

Vigogo kutoka Ujerumani Bayern Munich na Borussia Dortmund , timu zilizopambana katika fainali ya mwaka 2013 , pamoja na mabingwa watetezi Real Madrid zimekuwa katika hali nzuri sana katika kinyang'anyiro hicho msimu huu na zina matumaini ya kupata ushindi wa nne wakati wakipambana na timu walizozishinda ugenini wiki mbili zilizopita.

Real Madrid , ambayo inaongoza La Liga hivi sasa , inawakaribisha mabingwa mara tano wa kinyang'anyiro hicho cha vilabu vya Ulaya Liverpool katika kundi B , baada ya kushinda kwa mabao 3-0 uwanjani Anfield wakati wa mchezo wa tatu.

Mannschaftsfoto Real Madrid 16.09.2014
Mabingwa watetezo Real Madrid wanachuana na LiverpoolPicha: imago

Shauku kubwa katika kundi hilo inaonekana kuwa nani anaweza kumaliza wa pili , wakati timu tatu zote zina pointi tatu. Bassel na Ludogorets zinaumana nchini Uswisi kesho Jumanne baada ya Wabulgaria kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo uliopita.

Borussia Dortmund inapitia kipindi cha kushangaza msimu huu ambapo inaonekana kuyumba sana katika ligi nyumbani wakati imeweza kuwapiga kikumbo wapinzani wake wote hadi sasa katika Champions League katika kundi D.

Iwapo kikosi cha Jurgen Klopp na Arsenal zitashinda michezo yao kesho Jumanne , Arsenal ikipambana na Anderlecht , timu zote zitakuwa zimekata tikiti ya kuingia awamu ya mtoano ya timu 16 barani Ulaya.

Bayer Leverkusen inaongoza kundi C , na inamiadi na Zenit St Petersburg kesho Jumanne, na iwapo Leverkusen itateleza dhidi ya Warusi itaporomoka katika nafasi ya pili. Monaco ambayo iko nafasi ya pili katika kundi hilo la C inakwaana na Benfica Lisbon

Jumatano itakuwa zamu ya timu nyingine mbili za Ujerumani kujaribu kukata tikiti kuingia katika awamu ya makundi. wakati bayern Munich ina hakika ya kufanya hivyo baada ya kuikandika AS Roma kwa mabao 7-1 wiki mbili zilizopita, inaikaribisha timu hiyo katika uwanja wa Allianz Arena na hakuna anayefikiri kuwa kutatokea mapinduzi katika pambano hilo.

Mannschaftsfoto FC Barcelona 21.10.2014
Kikosi cha BarcelonaPicha: picture alliance/ZUMA Press

Schalke 04 nayo itakuwa ugenini ikiwa wageni wa Sporting Lisbon baada ya pambano lao wiki mbili zilizopita kuishia kwa ushindi wa mabao 4-3 mjini Gelsenkirchen mara hii pambano hilo litakuwa na mvuto wa aina yake baada ya Schalke kupata penalti dakika za mwisho ambayo imezusha gumzo kubwa iwapo ilikuwa halali ama la.

Chelsea iko njiani kuitembelea Maribor ya Slovenia , baada ya kuwaswaga kwa mabao 6-0 wiki mbili zilizopita. Barcelona nayo ni wageni wa Ajax Amsterdam katika kundi F ambapo iko nyuma ya Paris St German kwa pointi moja.

Kocha ambaye amefanikiwa kushinda kombe la dunia akiwa na kikosi cha Italia Marcello Lippi ameashiria kuwa anafikia mwisho wa kibarua hicho cha ukocha baada ya kuiongoza Guangzhou Evergrande kupata ubingwa wake wa nne mfululizo katika ligi ya China , Super League. Nafasi ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 66 , itachukuliwa na Fabio Cannavaro nahodha wa timu ya Italia iliyotwaa kombe la dunia nchini Ujerumani mwaka 2006.

Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe / zr
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman