1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tisa wauwawa na wengine 40 kujeruhiwa nchini Libya

13 Juni 2011

Waasi wa Libya wanaojaribu kusonga mbele kuelekea mji mkuu wa Tripoli leo wamekabiliana vikalo na wanajeshi watiifu kwa Kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi huko upande wa mashariki mwa nchi hiyo

https://p.dw.com/p/11ZYh
Waasi wa LibyaPicha: picture alliance / dpa

Kwa mujibu wa taarifa ya kituo cha televisheni cha Al Jazeera, waasi kwa hivi sasa wanaelekea Zlitan, mmoja katika ya miji mitatu inayotenganisha mji unaoshikiliwa na waasi wa Misrata na Tripoli ambapo bado Gaddafi anaendelea kudhibiti.

Jana watu tisa waliuwawa katika mji mwingine unaoshikiliwa na waasi wa Zintan baada wanajeshi wa Gaddafi kuwashambuliwa kwa makombora ya maroketi na vifaru ambapo wengine 40 wamejeruhiwa.

Libyen Westerwelle und Niebel
Waziri wa Mamno ya Nje wa Ujerumani na Guido na wa Maendeleo ya Kimataifa Dirk Niebel wakiwasili mjini BenghaziPicha: picture-alliance/dpa

Katika hatua nyingine, Ujerumani imeilitambua Baraza la Waasi Nchini Libya, kama chombo halali kinachowawakilisha wananchi wa nchi hiyo. Kauli hiyo imetolewa leo hii mjini Benghazi na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle.

Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya mkutano wake na maafisa wa baraza hilo, akiwemo pia Waziri Mambo ya Nje wa baraza hilo, Ali al-Essawi, Westerwelle amesema " wanataka Libya huru, yenye amani na demokrasia, pasipo Muammar Gaddafi.

Awali Deutschwelle ilizungumza kwa njia ya simu na mshauri wa siasa wa Baraza la Mpito la Waasi kutoka Benghazi, Mahmud Jibril, ambae alielezea matarajio yao kutoka kwa Ujerumani hasa baada ya kuondoka kwa Gaddafi madarakani." Tungelipenda kuwa na uhusiano mzuri na Ujerumani, tungelipenda pia kuboresha huu uhusiano katika siku zijazo, tuna miradi ambayo ilianzishwa hapo awali kwa ushirikiano wa serikali ya Ujerumani, wakati wa utawala wa Gaddafi na tungependa sana miradi hii iendelee, na tungelipenda kufanya makubaliano mapya kuhusu miradi hii tena"

Ujerumani imekuwa nchi ya 13 kulitambua baraza la waasi kama chombo kinachowakilishwa wananchi, ambapo awali zilikuwa Australia, Uingereza, Ufaransa, Gambia, Italia na Jordan.

Nchi nyingine pia ambazo zimekwishalitambua baraza hilo la waasi ni Malta, Qatar, Senegal, Uhispania, Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kutokana na uamuzi huo wa kulitambua baraza la waasi, Umoja wa Falme za kiarabu leo umetoa masaa 72 kwa balozi wa Libya katika nchi hiyo kuondoka.

Libyen Muammar Gaddafi Moammar Gadhafi
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: picture-alliance/dpa

Ama katika hali isiyo ya kawaida, jana televisheni ya Libya ilimuonesha kiongozi wa Libya akikutana na rais wa chama cha kimatiafa cha mchezo wa chess.

Shirika la Habari la Urusi limemnukuu Kirsan IIyumzhhiinov, ambae pia aliwahi kuwa gavana nchini Urusi, akisema alicheza chess na Gadaffi hapo jana, na kuongeza kwamba kiongozi huyo amesema hana mpango wa kuondoka nchini humo.

Gaddafi amekuwa madarakani kwa miaka 42. Vurugu nchini humo zilianza katikati ya Februari baada ya serikali kutumia nguvu kuwakandamiza waandamanaji.

Mwandishi: Sudi Mnette/ AFP/RTR

Mhariri:Miraji Othman