1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Tishio la ugaidi ni kubwa katika eneo la migogoro la Afrika

Tatu Karema
2 Februari 2024

Tishio la kigaidi kutoka kwa kundi la al-Qaida na lile linalojiita dola la kiislamu IS, limesalia kuwa juu katika maeneo yenye migogoro barani Afrika na ndani ya Afghanistan

https://p.dw.com/p/4bxM4
Wanachama wa kundi la al-Qaeda wakibeba bunduki aina ya AK-47 katika video iliyochapishwa na Osama bun Laden mnamo mwaka 2001
Wanachama wa kundi la al-Qaeda wakibeba bunduki aina ya AK-47Picha: AFP/Getty Images

Katika ripoti ya kurasa 23, iliyotumwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, jopo la wataalamu wa Umoja huo, limesema kuwa uhusiano kati ya watawala wa Taliban wa Afghanistan na al-Qaida bado ni wa karibu, na nchi wanachama ambazo hazikutajwa zinaripoti kuwa idadi kubwa ya makundi ya kigaidi nchini Afghanistan inahujumu hali ya usalama katika eneo hilo.

Soma pia: Wataalamu wa UN wasema makundi ya kigaidi yana uhuru Afghanistan

Ripoti hiyo inayoangazia hali hiyo ya usalama kufikia Desemba 16, 2023, inasema kuwa tishio kubwa zaidi ndani ya Afghanistan bado ni kutoka kwa kundi la IS lenye uwezo wa kuenea katika kanda hiyo na zaidi.

Makundi ya kigaidi yana malengo ya kutanuka ulimwenguni

Kikanda, wataalamu hao walitaja mfululizo wa mashambulizi katika mataifa jirani ya Iran na Pakistan na vitisho katika mataifa ya Asia ya Kati.

Hata hivyo, jopo hilo linasema, kuwa wakati ambapo hakuna hata kundi moja lenye mafungamano na al-Qaidaambalo limepata uwezo wa kufanya mashambulizi kwenye maeneo ya mbali na yalipo, bado lakini yana malengo ya kutanuka ulimwenguni.

Soma pia:Umoja wa Mataifa yasema kundi la IS lingali kitisho

Jopo hilo limesema kuwa nguvu ya IS katika nchi hizo mbili bado iko kati ya wapiganaji 3,000 na 5,000. Nchini Iraq, wanafanya uasi wa kiwango kidogo na makundi mengine yenye ushirika nayo,  wakati nchini Syria, mashambulizi yameongezeka tangu mwezi Novemba.

Wataalamu hao wameongeza kuwa kuchelewa kwa miezi mitatu kumtaja kiongoziwa sasa wa IS, Abu Hafs al-Hashemi al-Qurayshi, kufuatia kifo cha mtangulizi wake asiyejulikana sana, kunachukuliwa kuwa ishara ya matatizo ya ndani na changamoto za kiusalama.

Wanajeshi wa ujumbe wa Ufaransa unaojulikana kama Barkhane katika operesheni iliyoanza Agosti 1 mwaka 2014  dhidi ya waasi katika eneo la Sahel
Wanajeshi wanashika doria dhidi ya magaidi katika eneo la SahelPicha: Philippe De Poulpiquet/MAXPPP/dpa/picture alliance

Baadhi ya mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo hayakutajwa yametathmini kuwa shinikizo kubwa kutokana na operesheni za kukabiliana na ugaidi nchini Syria na Iraq huenda kukahamisha uongozi wake na kitovu chake barani Afrika au Afghanistan, huku Afrika ikiwa na uwezekano mkubwa.

Soma pia:UN: Taliban bado ina mahusiano na Al-Qaida

Katika eneo la Afrika Magharibi na Sahel, wataalamu hao wamesema kuwa vurugu na vitisho vimeongezeka tena katika maeneo yenye migogoro, na kuzua wasiwasi miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa.

al-Shabab bado inajikakamua

Katika eneo la Afrika mashariki, wataalam hao wamesema kuwa serikali ya Somalia inaendeleza mashambulizi yake ya kijeshi dhidi ya kundi la al-Shabab, lenye mafungamano na al-Qaida, lakini mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa yanatathmini kwamba licha ya hasara kubwa kutokana na mashambulizi ya anga na operesheni za kijeshi, kundi al-Shabab bado linajikakamua.

Tishio la ugaidi laongezeka Ulaya

Barani Ulaya, wataalamu hao wanasema kuwa viwango rasmi vya tishio la ugaidi vimeongezeka . Hii ni kufuatia mashambulizi mabaya mwishoni mwa 2023 nchini Ufaransa na Ubelgiji, pamoja na matukio mengi ya kigaidi ambayo hayakusabibisha mauaji na pia kukamatwa kwa watu kadhaa katika mataifa ya eneo hilo.