1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tohara ya Wanaume yathibitishwa kusaidia kuzuia maambukizi ya HIV

Saumu Mwasimba24 Julai 2007

Je wewe ulikuwa unajua kwamba kutahiri kwa wanaume kunaweza kusaidia kuzuia hatari ya maambukizi ya virusi vya HIV?

https://p.dw.com/p/CB2V
Vifo vinavyotokana na ukimwi vinaweza kupungua
Vifo vinavyotokana na ukimwi vinaweza kupunguaPicha: AP

Hayo yamebainishwa na mtafiti mmoja kutoka Marekani Richard Bailey katika mkutano unaojadili juu ya maradhi ya Ukimwi huko Sydney Ausralia.

Richard Bailey mtafiti wakimarekani amezitaka nchi mbali mbali kupigia upatu suala hilo la kutahiri wanaume akisema uchunguzi wa kisayansi umeonyesha wazi kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa mtu aliyetahiriwa kuepuka maambukizi ya virusi vya Hiv kuliko kwa mtu ambaye hajatahiri.

Mtafiti huyo kutoka jimbo la Illinois nchini Marekani ameuambia mkutano wa Sydney unaojadili kuhusu maradhi ya Ukimwi kwamba tohara inaweza kusaidia mamilioni ya watu wasiambukizwe virusi vya Hiv katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa matibabu nchini Kenya Dkt James Nyikal uchunguzi uliofanywa katika mataifa ya Afrika Kusini,Kenya na Uganda umebainisha ni kweli tohara inaweza kusaidia pakubwa katika kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya HIV.

Utafiti huo uliofanyika Kenya, Afrika Kusini na Uganda ulisimamishwa kabla ya kukamilika kutokana na matokeo yake kutoa tamaa zaidi na kuhofiwa kwamba huenda wanaume wakajitumbukiza kwenye tendo la ndoa bila kujali tena wakiiamini wameshapata kinga asilia ‘’Natural Condom’’.

Hata hivyo mtaalamu Bailey kutoka Marekani anasema serikali ya kiafrika lazima zisimame kidete kuzungumzia umuhimu wa tohara kwa wanaume katika mataifa yao ili kukabiliana na janga la Ukimwi kwa sababu wataalamu wa afya wa kimataifa hawawezi kulazimisha juu ya suala hilo hii ni kwasababu huenda wakaonekana ni watu wanaotaka kuingilia tamaduni Fulani za jamii za waafrika.

Katika mkutano huo wa Sydney pia imebainika wanawake wengi barani Afrika hutumia limao au ndimu kujisafisha baada ya tendo la ndoa ili kuepuka kupata virusi vya Hiv lakini hilo halijasaidia kitu.

Mtafiti kutoka Nigeria Atiene Sagay amesema utafiti huo uliofanywa kwa zaidi ya makahaba 300 nchini mwake ulibainisha kuwa wanawake hao hawakusalimika kuambukizwa virusi vya HIV.

Kiasi cha wanaume millioni 665 takriban asilimia 30 duniani wamepashwa tohara.Barani Afrika kiasi cha asilimia 68 wametahiriwa kutokana aidha na mila na desturi au dini na wala sio kwa sababu ni tendo linalosaidia kiafya.