1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TOKYO: Rice azuru Japan

18 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD1b

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Bi Condoleezza Rice amewasili mjini Tokyo Japan, kituo chake cha kwanza katika ziara yake ya Asia. Lengo kubwa la ziara yake ni kujadili utekelezaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.

Akizungumza mjini Tokyo hii leo, Condoleezza Rice amesema Marekani itatimiza kikamilifu jukumu lake la usalama kwa Japan.

´Marekani inataka na ina uwezo wa kutimiza kikamilifu jukumu lake la usalama kwa Japan.´

Ziara yake inafanyika wakati wasiwasi ukizidi kwamba Korea Kaskazini huenda inajiandaa kufanya jaribio la pili la zana za kinyuklia.

Condoleezza Rice anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na mawaziri wa ulinzi na mambo ya kigeni wa Japan. Bi Rice atazuru pia Korea Kusini, China na Urusi.

Wakati huo huo, mjumbe wa Marekani katika mzozo wa nyuklia, naibu waziri wa mambo ya kigeni, Chistopher Hill, amewasili pia mjini Tokyo hii leo. Hill amesema Marekani italichukulia jaribio la pili la Korea Kaskazini kama jibu la uchochezi wa vita kwa jamii ya kimataifa.

´Nafikiri jamii ya kimataifa haitakuwa na chaguo lengine bali kuchukua hatua kali kabisa dhidi ya utawala wa Korea Kaskazini.´

Christopher Hill amewaambia waandishi habari anataka kukutana na maofisa wa Korea Kusini juu ya data za setelaiti zinazoonyesha kwamba Korea Kaskazini inajiandaa kufanya jaribio la pili la zana za kinyuklia.