1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TOKYO: Shinzo Abe akataa kung´atuka

30 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBdl

Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe, ameapa hatajiuzulu wadhifa wake licha ya muungano wake kushindwa vibaya kwenye uchaguzi wa baraza la juu la bunge uliofanyika jana nchini humo.

Chama cha upinzani cha Democtratic Party of Japan, kilishinda idadi kubwa ya kura na kitakuwa chama kikubwa katika baraza hilo kwa mara ya kwanza.

Chama cha Shinzo Abe bado kina idadi kubwa ya wabunge kwenye baraza dogo la bunge. Matokeo ya uchaguzi huo yameifanya serikali ya waziri mkuu, Shinzo Abe, kutiliwa shaka na miito imetolewa kumtaka kiongozi huyo ajiuzulu.

Akizungumza juu ya matokeo ya uchaguzi huo Shinzo Abe amesema, ´Nitayakubalia matokeo ya uchaguzi huu na kuyazingatia sana. Lakini wakati huo huo, nitajaribu kutimiza ahadi yangu ya kujenga nchi mpya na kuendeleza mageuzi.´

Waziri mkuu Shinzo Abe ameahidi kufanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri ili kupunguza hasira miongoni mwa wapigaji kura. Amepuuza miito ya kumtaka aitishe uchaguzi wa mapema wa baraza la chini la bunge ili aweze kujiimarisha kisiasa.

Shinzo Abe amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kumtaka ajiuzulu ndani ya chama chake lakini wachambuzi wanasema huenda akaendelea kubakia madarakani kwa kukosekana mtu anayefaa kuichukua nafasi yake.