1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Toure ajiunga na kampeni ya kuwaokoa tembo

29 Oktoba 2013

Mchezaji ambaye anamiliki taji la sasa la mwanasoka bora wa mwaka barani Afrika, Yaya Toure, amechaguliwa kuwa balozi wa Shirika la Kuhifadhi Mazingira la Umoja wa Mataifa – UNEP

https://p.dw.com/p/1A7vM
Picha: picture alliance/dpa

Tpure amepewa jukumu la kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu. Nyota huyo wa klabu ya Manchester City na timu ya taifa ya Cote d'Ivoire ameonya kuwa uwindaji haramu wa pembe za ndovu unatishia kuangamiza wanyama hao. Akizungumza mjini Nairobi baada ya kupewa wadhifa wa kuwa Balozi wa UNEP, Toure amesema kama hatua haitachukuliwa sasa, huenda mnyama huyo akatoweka kabisa katika siku za usoni.

Aliongeza kuwa timu ya kandanda ya Cote d'Ivoire inafahamika kama "The Elephants" kama heshima kwa wanyama hao ambao wana nguvu na neema, na ilhali nchini mwake pekee kuna tembo 800 tu waliobaki.

Akizungumza katika makao makuu ya UNEP mjini Nairobi, Kenya, Toure amesema anataka kusaidia kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu ambayo husababisha maelfu ya ndovu kuwindwa na kuuawa kila mwaka.

Ujangili umeongezeka kwa kiasi kikubwa barani Afrika katika miaka ya karibuni na biashara haramu ya pembe za ndovu imeongezeka mara tatu tangu mwaka wa 1998, kwa mujibu wa UNEP.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Josephat Charo