1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Transparency International latoa ripoti kuhusu ufisadi duniani.

26 Oktoba 2010

Denmark na Singapore zina visa vichache vya ufisadi ilhali Afghanistan, Somalia na Iraq zinaongoza kwa ufisadi.

https://p.dw.com/p/Po9n
Shirika la Transparency International limeelezea wasiwasi wake kutokana na kuongezeka kwa ulaji rushwa duniani.

Denmark na Singapore ni kati ya mataifa yenye visa vichache kabisa vya ufisadi duniani, ilhali Afghanistan na Iraq ndiyo yanazongwa na rushwa kwa kiwango cha juu. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka iliyotolewa leo na shirika la kutathmini viwango vya ufisadi duniani, Transparency International.

Kulingana na ripoti iliyotolewa rasmi mjini Berlin hapa Ujerumani leo, shirika la Transparency International linalodurusu ufanisi wa mataifa duniani yanavyopiga vita ufisadi, theluthi tatu ya mataifa 178 yaliyofanyiwa uchunguzi yalikuwa na alama chini ya wastani, ikiwa sifuri huashiria kiwango cha juu kabisa cha ufisadi na kumi ni kiwango cha chini kabisa cha visa vya ufisadi.

Rais wa shirika hilo, Huguette Labelle, amesema matokeo ya ripoti hiyo yanaonesha kwamba kuna tatizo sugu la ufisadi na ulaji rushwa. Bibi Labelle amesema kuruhusu ufisadi kuendelea hakutakubalika kamwe kwa sababu watu wengi maskini wanaendelea kuteseka kutokana na athari yake kote duniani.

Somalia na Afghanistan ndizo nchi zenye visa vingi na kiwango kikubwa kabisa cha ufisadi duniani cha alama 1.1, zikifuatiwa na Myanmar kisha Iraq katika nafasi ya nne.

Kulingana na ripoti hiyo, kwa upande mwingine, Denmark, New Zealand na Singapore ndizo nchi ambazo zina visa vichache zaidi vya rushwa, vikiwa na alama 9.3.

Katika kiwango hicho, Finland, Sweden, Canada na Uholanzi pia zimejizatiti kuhakikisha ufisadi unazuiwa.

Chile, Equador, Macedonia, Kuwait na Qatar yametajwa kama mataifa ambayo yamepiga hatua kubwa kwa kuwa na sera zisizoendeleza ufisadi.

Tofauti na hayo, Jamhuri ya Czech, Hungary, Italy na Madagascar ni kati ya yale yanayopiga hatua moja mbele na mbili nyuma katika vita dhidi ya ufisadi. Marekani pia ipo katika kundi hilo na ni taifa la 22 duniani kulingana na kiwango chake cha ufisadi.

Shirika hilo la Transparency International, linakiri kwamba ufisadi unadumaza jitihada za kukabiliana na matatizo makubwa duniani yakiwemo mzozo wa kiuchumi na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.

Tamara Kamhawi ambaye ni mratibu wa shirika hilo katika kanda ya mashariki ya kati, aliiambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kwamba suala la rushwa ni kitisho kikubwa cha maendeleo katika kanda hiyo.

Mzozo wa kiuchumi duniani umelaumiwa kwa kuchangia mataifa kadhaa kuzongwa na visa vingi vya rushwa. Transparency International limetoa mwito kwa mataifa yanayoinukia kiuchumi katika kundi la G20, yakabiliane na tatizo la rushwa hasa baada ya mzozo wa kifedha.

Shirika hilo linalotathmini viwango vya rushwa katika mataifa 178 duniani kila mwaka, huwahusisha wataalam kutoka katika sekta 13 wakiwemo wafanyabiashara, wadadisi wa mwelekeo wa masoko na pia waandishi wa habari ili kuweza kupata takwimu linganishi vya viwango vya ufisadi duniani.

Mwandishi: Peter Moss /AFP/DPA

Mhariri: Othman Miraji