1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TRIPOLI : Ulaya yatakiwa kuacha kushinikiza kesi ya wauguzi

17 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCRW

Maafisa wa serikali ya Libya hapo jana wameonya kwamba shinikizo la Ulaya halisaidii kesi ya wauguzi sita wa Bulgaria na dakkari mmoja wa Kipalestina waliohukumiwa kifo katika kesi ya janga la UKIMWI.

Balozi wa zamani wa Libya kwa Uingereza Mohammed al Zuwi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba shinikizo la Ulaya na kuingilia kati kesi hiyo hakusaidii cho chote.

Badala yake amesema nchi hizo za Ulaya zinapaswa kutowa fedha kufidia familia za wahanga wa mji wa Benghazi.

Wauguzi hao watano na daktari wa Kipalestina walikamatwa hapo tarehe 9 Februari mwaka 1999 baada ya mamia ya watoto katika hospitali ya watoto ya Benghazi ambako walikuwa wakifanya kazi waliambukizwa virusi vya HIV vinavyosababisha UKIMWI.

Wana tiba hao wamekanusha tuhuma kwamba waliwaambukiza kwa makusudi zaidi ya watoto 400 na wamekuwa wakiungwa mkono katika rufaa yao na wataalamu wa kimataifa ambao wamesema maambukizi hayo yametokana na hali mbaya ya uchafu katika hospitali.