1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ahofiwa kuibua vita vya kibiashara

Lilian Mtono
8 Machi 2018

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Brigitte Zypries amesema vita vya kibiashara bado havijalipuka kufuatia mpango wa rais wa Marekani Donald Trump wa kupandisha ushuru wa bidhaa za chuma na bati zinazoingizwa nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/2tw2f
Simbabwe Alltag Fotoreportage von Cynthia R Matonhodze
Picha: DW/C. R. Matonhodze

Waziri wa uchumi wa Ujerumani Brigitte Zypries amesema hii leo kwamba vita vya kibiashara bado havijalipuka kufuatia mpango wa rais wa Marekani Donald Trump wa kupandisha ushuru wa bidhaa za chuma na bati zinazoingizwa nchini Marekani. Lakini amesema hatua ya Trump inakereketa, na Umoja wa Ulaya, EU unatakiwa kuutolea majibu. 

Akizungumza na kituo cha matangazo cha Ujerumani cha ARD, waziri Zypries alinukuliwa akisema, hawezi kueleza kama kuna vita dhahiri kwa wakati huu, akisema bado havijaanza, kwa kuwa zinazungumziwa bidhaa chache tu. Lakini aliongeza kuwa mapendekezo ya ushuru yalichangia kuongeza kile alichotaja kama "ukakasi".

Trump alitarajiwa kusaini tangazo la rais la kuanzishwa kwa ushuru huo hii leo, lakini maafisa wa Ikulu ya White House walisema kuna uwezekano wa kusogezwa mbele hadi kesho Ijumaa kwa sababu nyaraka za mpango huo zinatakiwa kwanza kupitia kwenye mchakato wa kisheria.

Waziri Zypries ameutaka Umoja wa Ulaya, kutoa majibu kuhusu hatua hiyo ya Trump ya kuanzisha ushuru huo, na italazimika kuwasilisha malalamiko katika shirika la kimataifa la biashara, WTO. Lakini pia amesisitizia umuhimu wa kuendeleza mazungumzo na serikali ya Marekani.

China, IMF na Umoja wa Ulaya wataka Marekani kujieousha na vita vya kibiashara.

Mjini Geneva, China imeeleza wasiwasi wake mbele ya shirika la biashara la dunia, WTO ambako wanachama wengine 17 wa shirika hilo wamepaza sauti kuhusiana na hatua hiyo. Msemaji wa WTO Keith Rockwell alisema wengi wameeleza hofu yao kuhusu visasi vya papo kwa papo, vinavyoweza kusambaa na kushindikana kudhibitiwa, hatua inayoweza kuathiri uchumi wa dunia na mfumo wa biashara za kimataifa.

Peking PK Wang Yi Außeniminister China
Waziri wa mambo ya nje ya China Wang Yi amesema China itazungumzia suala hilo kutakapokuwa na umuhimu.Picha: picture-alliance/dpa/X. Guangli

Leo Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi,  amesema nchi yake itaweza kujibu kuhusiana na suala hilo la vita vya kibiashara na Marekani iwapo kutakuwa na umuhimu .

Wang amesema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya mkutano mkuu wa bunge la China, na kuongeza kuwa Marekani na China hawakutakiwa kuwa wapinzani, na historia imeonyesha kwamba vita vya kibiashara havikuwahi kuwa hatua sahihi ya kusaka suluhu ya matatizo.

Umoja wa Ulaya na shirika la la kimataifa la fedha, IMF pia zimemtaka rais Donald Trump kujiepusha na hatari ya vita vya kibiashara, baada ya kujiuzulu kwa mshauri wake mwandamizi wa uchumi, hatua iliyooongeza msukumo kwa kundi  linaomuunga mkono kuendelea na mpango wake huo wa kuweka ushuru kwenye bidhaa hizo za chuma na bati.

Kulingana na mkuu wa IMF, Christine Lagarde, hapo jana alisema katika kile kinachoelezwa kama vita vya kibiashara, hakuna mshindi, na badala yake pande zote hushindwa, na kuongeza kwamba vita vya kibiashara vinaweza kusababisha kuongezeka kwa wasiwasi katika ukuaji wa uchumi wa dunia. 

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kusaini kuanzishwa kwa ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa ya chuma na bati zinazoingizwa nchini humo wiki hii. Hatua kama hiyo inalenga kukabiliana na uingizwaji wa bidhaa za viwango duni, hususan kutoka China, ambazo kulingana na Trump ni kwamba zinadidimiza sekta ya viwanda na ajira nchini Marekani.

Mwandishi: Lilian Mtono/rtre.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman