1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aiweka Iran katika "ilani"

Iddi Ssessanga
2 Februari 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran imewekwa katika "ilani" baada ya jaribio la karibuni la kombora, na kudai kwamba nchi hiyo ilikuwa kwenye kingo za kuporomoka wakati iliposaini makubaliano ya nyuklia.

https://p.dw.com/p/2WsAQ
Iran Abschuss Emad Ballistische Rakete
Picha: picture-alliance/dpa/Iran Defense Ministry

Akirejea matamashi sawa na yaliotolewa na mshauri wake wa masuala ya usalama Michael Flynn siku moja kabla, Trump aliandika kwenye ukurasa wake twita mapema leo kwamba: "Iran imewekwa rasmi kwenye Ilani kwa kufyatua kombora la masafa marefu. Ilipaswa kuwa na shukrani kwa makubaliano mabaya Marekani iliosaini nao!"

Lakini ikulu ya White House haijatoa ufafanuzi wa nini hasa maana ya onyo hilo kivitendo, na bado haijajulikana iwapo ikulu hiyo itataka kuiwekea Iran vikwazo safari hii. Flynn alisisitiza kwamba jaribio hilo la kombora lililofanyika siku ya Jumapili lilikuwa ukiukaji wa azimio la Umoja wa Mataifa nambari 2231, linaloitaka Iran kutojaribisha makombora yenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia.

'Iran ilikuwa hoin bin taabani'

Trump na Flynn wamekuwa wakosoaji wakubwa wa serikali ya mjini Tehran na wapinzani wa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na mataifa makubwa, yaliopelekea Iran kuzuwia mpango wake wa nyuklia na badala yake ikalegezewa vikwazo. Trump alisema katika tweet yake ya pili alfajiri kwamba Iran ilikuwa hoi ikisubiri tu kuporomoka, wakati Marekani ilipokuja kuinusuru kupitia makubaliano hayo yalioihakikishia kiasi cha dola bilioni 150 katika kulegezewa vikwazo.

USA Michael Flynn
Mshauri wa masuala ya usala wa Trump Michael Flynn.Picha: Reuters/C. Barria

Lakini mshauri wa juu wa kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema siku ya Alhamisi kuwa Iran haiwezi kutishwa na kauli za vitisho za Marekani kuhusiana na jaribio lake la kombora zinazotolewa na rais asiyekuwa na uzoefu wowote. Iran ilikiri jana kuwa ilifanya jaribio la kombora hilo lakini ikasema jaribio hilo halikukiuka makubaliano kati yake na mataifa sita makubwa, au azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Mshauri huyo wa Khamenei  Ali Akbar Velayati, alinukuliwa na shirika la habari la Fars akisema "hii siyo mara ya kwanza kwa mtu asie na uzowefu kuitishia Iran", na kuongeza kuwa serikali ya Marekani itafahamu kuwa kuitishia Iran hakuna maana yoyote. Afisa wa Marekani alisema kombora hilo la Iran lilisafiri umbali wa kilomita 1,010, madai ambayo Iran iliyakanusha.

Msigano kati ya Trump na waziri mkuu Australia

Wakati huo huo gazeti la Washington Post, likinukuu duru kutoka serikali ya Marekani, limeripoti kuwa Trump alimkaripia vibaya waziri mkuu wa Australia Malcom Turnbull wakati wa mazungumzo yao ya kwenye simu siku ya Jumapili, na kufikia hatua ya kumkatia simu kiongozi huyo wa taifa mshirika wa Marekani, kuhusiana na makubaliano juu ya Marekani kuwapokea wakimbizi waliokataliwa na Australia, ambao kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliofikiwa wakati wa utawala wa Obama, Marekani inatakiwa kuwachukuwa.

Imeripotiwa kuwa Trump aliitaja simu aliompigia Turnbull kuwa mbaya zaidi kati ya simu nne aliozowapigia viongozi wa dunia siku hiyo.

Ingawa waziri mkuu Turnbull alisema mazungumzo kati yake ya Trump yalikuwa ya kirafiki, na kwamba rais huyo alikubali kuheshimu makubaliano hayo na pia msemaji wa White House Sean Spicer kuthibitisha hivyo, Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa twita na kuyashambulia vikali makubaliano hayo na kuyataja kuwa ya kijinga na kuahidi kuyapitia upya. Turnbull anakusha kuwa Trump alimkatia simu na kusema anasikitika kwamba mazungumzo yake na Trump yalivujishwa.

Australien Premierminister Malcolm Turnbull mit Smartphone
Waziri mkuu wa Australia Malcom TurnbullPicha: Reuters/AAP/Lukas Coch

"Nimesikitishwa sana kwamba kumevujishwa kile kinachodaiwa kuwa mazungumzo yetu ya simu mjini Washington. Lakini nataka niseme kitu kimoja kuhusu suala hilo. Ripoti kwamba Rais Trump alikataa simu siyo sahihi. Simu hiyo ilimalizika vizuri na kulingana na mazunungumzo yenyewe, yalikuwa ya wazi na kirafiki. Nawakilisha maslahi ya Australia. Natoa hoja za Australia kwa nguvu na kushawishi kadiri niwezavyo, popote ninapokuwa."

Wasaidizi wa Trump hawaijui EU

Mratibu wa serikali ya Ujerumani wa masuala ya mataifa ya Atlantic Jürgen Hardt, amesema watu wanaomzunguka trump wana ufahamu kidogo kuhusu Umoja wa Ulaya, na kwamba Ujerumani inapaswa kuelezea namna kanda hiyo kubwa zaidi ya kibiashara duniani inavyofanya kazi.

Akiongea baada kufanya mazungumzo na maafisa waandamizi katika ikulu ya White House, Hardt aliliambia gazeti la Der Tagessspiegel, kwamba inaonekana utawala mpya Marekani unalena kuwa mahusiano na taifa mmoja mmoja na Umoja wa Ulaya.

Mapema jarida la Marekani la World Trade Online liliripoti kwamba mataifa kadhaa ya Umoja wa Ulaya yalikataa maombi ya utawala wa trump kujadiliana nayo mmoja mmoja mikataba ya kibiashara.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe,dpae

Mhariri: Saumu Yusuf