1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amtema Bannon

Mohammed Khelef
19 Agosti 2017

Rais Donald Trump ametengana rasmi na mkuu wake wa mkakati mwenye utata, Steve Bannon,  wakati Ikulu ya White House ikikumbwa na ukosoaji mkubwa kutokana na kauli za Trump juu ya maandamano ya Charlottesville.

https://p.dw.com/p/2iUac
Stephen Bannon
Picha: picture alliance/AP Photo/A. Brandon

Hata hivyo, Bannon mwenye umri wa miaka 63, ambaye kuondoka kwake siku ya Ijumaa (18 Agosti) kunaongezea orodha ya majanga makubwa kwenye utawala mchanga wa Trump ndani ya wiki kadhaa sasa, aliapa kwamba ataendelea kushinikiza ajenda ya siasa kali za mrengo wa kulia, wakati akirejea kwenye mtandao wake wa habari wa Breibart News, mashuhuri kwa siasa kali za wahafidhina mamboleo.

"Ikiwa kuna mkanganyiko wowote, wacha niweke wazi: ninaondoka White House na kwenda vitani kwa ajili ya Trump dhidi ya wapinzani wake bungeni, kwenye vyombo vya habari na Marekani inayomilikiwa na mashirika makubwa," mtu huyu anayetambuliwa kama 'shujaa' na makundi ya siasa kali aliiambia televisheni ya Bloomberg masaa machache baada a kuondoka White House.

Kuondoka kwa Bannon kunaashiria ukubalifu wa utawala wa Trump kuridhia mabadiliko yanayotakiwa na wabunge wa chama chake cha Republican kwenye duara linalomzunguka kiongozi huyo, hasa kwa wabunge hao kutoridhishwa na siasa zao zinazokinzana na misingi inayoitambulisha Marekani. 

Bado haijafahamika lipi litakuwa jukumu la mwanamikakati huyo, ambaye anasifiwa kwa kuisaidia kampeni ya ushindi ya Trump, atalitekeleza akiwa nje ya White House.

Kuongoza vuguvugu la siasa kali za kibaguzi

Donald Trump wa Marekani
Hatimaye Rais Donald Trump amelazimika kutengana na mtu aliyemuingiza Ikulu ya White House.Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Katika maoni yake kwa gazeti la Weekly Standard, aliweka wazi utayari wake wa kuendelea na vuguvugu la siasa kali za kizalendo, ambalo ndilo lililomuweka Trump madarakani.

"Urais wa Trump tulioupigania na kushinda, sasa umekwisha," alisema. "Bado tuna vuguvugu kubwa, na tuliutengeneza huu urais wa Trump. Lakini urais huo umekwisha. Kitakuwa kitu chengine tafauti sasa."

Kuwepo kwa Bannon kwenye ofisi ya rais wa Marekani tangu awali kulikuwa kukipingwa vikali, na wakati Trump mwenyewe akiwa ameelemewa na ukosoaji mkubwa kwa kuwafananisha waandamanaji wanaopinga ubaguzi na wale wanaoutukuza kuwa wote ni wa kulaumiwa kwa ghasia za Charlottesville, Virginia, inaelekea rais huyo alishindwa na shinikizo na akamuwacha mshirika wake aende.

Trump, ambaye alijipatia umaarufu wa kisiasa kwa kujenga shaka endapo Barack Obama, rais wa kwanza mweusi nchini Marekani, alizaliwa nchini humo, awali alikuwa amewalaani wafuasi wa unazi mamboleo na kundi la Ku Klux Klan, lakini siku moja baadaye akajitenga mbali na kauli yake ya mwanzo, na kuja na mfananisho wa kimaadili kati ya makundi hayo mawili ya waandamanaji. 

"Kufutwa kazi kwa Steve Bannon ni habari njema, lakini haitafautishi na pale aliposimamia rais mwenyewe kuhusiana na Wazungu wajionao peke yao ndio bora na imani za kipotofu wanazozitetea," alisema kiongozi wa wabunge wa Democratic, Nancy Pelosi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Isaac Gamba