1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amteua Thomas Bossert kuwa mshauri wa usalama wa ndani

Isaac Gamba
28 Desemba 2016

Rais Mteule wa Marekani Donald Trump hapo jana amemteua mmoja wa waliokuwa wasaidizi katika serikali ya Rais wa zamani wa Marekani  George W. Bush kuwa mmoja wa wasaidizi wake katika masuala ya usalama.

https://p.dw.com/p/2Uwxd
Donald Trump wendet sich an die Presse in Palm Beach Florida
Picha: Reuters/C. Barria

Thomas Bossert  ambaye awali alikuwa  mmoja wa watu wa karibu wa Trump katika masuala yake ya kibiashara atakuwa sasa msaidizi wa Trump katika masuala ya usalama wa ndani pamoja na masuala ya kupambana na ugaidi. Taarifa kutoka katika kamati ya mpito ya Trump imesema Bossert atakuwa akimshauri Trump katika masuala zaidi yanayohusu usalama wa ndani, usalama wa mitandaoni na kuratibu masuala yote yanayohusu utekelezaji wa sera zinazohusiana na usalama wa ndani katika ngazi ya baraza la mawaziri. Hata hivyo awali watunga sera nchini humo kwa muda mrefu wamekuwa wakishauri kuwa majukumu kama hayo yanayohusu usalama wa taifa yalipaswa yatenganishwa na ikulu ya White House.

 Aidha Bossert pia anatarajiwa kufanya kazi kwa karibu zaidi na Trump akishirikiana na mshauri mwingine wa masuala ya usalama wa ndani Luteni Jenerali Michael Flyn. Bossert amewahi kuwa msaidizi wa rais wa zamani wa Marekani George W. Bush akimshauri kuhusiana na masuala ya usalama wa ndani.

Ama kwa upande mwingine Trump pia amemteua mmoja wa washauri wake wakuu katika masuala ya uhusiano kati ya Marekani na Israel Jason Greenblatt kuwa mwakilishi maalumu katika majadiliano kwenye ngazi ya kimataifa. Greenblatt amewahi pia kufanya kazi katika makampuni ya kibiashara ya Trump kwa zaidi ya miongo miwili na kwa sasa ni mmoja wa watendaji waandamizi na mshauri wa masuala ya kisheria katika makampuni hayo.

Katika taarifa yake rais huyo mteule wa Marekani amesema Bwana Greenblatt ana uzoefu wa kutosha katika kushiriki majadiliano yanayohusu mikataba mbalimbali na amekuwa akifanya kazi hizo kwa niaba yake na kuongeza kuwa ana uwezo pia kuzileta pamoja  na hatimaye kuweza kufikia makubaliano ya masuala mbalimbali mazito yanayozihusu pande tofauti. 

Trump pia hivi karibuni amemteua mmoja wa washauri wake waandamizi katika masuala yahusuyo uhusiano kati ya   Marekani na Israel kuwa balozi wa Marekani nchini Israel.

Tayari amemteua mkuu wa utumishi katika ikulu ya White House

USA Reince Priebus neuer Stabchef im Weißen Haus
Mkuu wa utumishi katika ikulu ya White House,Reince Priebus.Picha: Reuters/M. Segar

Uteuzi mwingine ambao tayari umefanywa na Trump hadi sasa ni pamoja na mkuu wa masuala ya utumishi katika ikulu ya White House, Reince Priebus na Steve Bannon ambaye alimteua kuwa mshauri wake mwandamizi. Mkwe wa Trump Jared Kushner ambaye anaelezwa kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika timu ya Trump pia anatarajiwa kuwa mmoja wa watu wa karibu kama wasaidizi wa rais huyo mteule.

Trump anaelezwa kuwa amekuwa akisababisha mgongano miongoni mwa wasaidizi wake katika makampuni yake ya kibiashara kwa maslahi yake binafsi hali ambayo inatia hofu kuwa iwapo atafanya hivyo tena katika ikulu ya White House basi itasababisha mkanganyiko na kuchelewesha katika kufanya maamuzi.

Wakati huo huo hapo jana maafisa wa polisi nchini Marekani walifanya upekuzi katika eneo la mapokezi lililoko katika jengo la Trump Tower kufuatia kuwepo kwa begi dogo la mgongoni katika eneo hilo ambalo halikuwa na mtu na kusababisha watu kuhofia usalama wao na kukimbia kutoka katika eneo hilo.

Hata hivyo maafisa hao wa polisi wanaohusika na masuala ya mabomu walibaini kuwa hakukuwa na kitisho chochote  dhidi ya usalama katika eneo hilo. Trump ambaye kwa sasa yuko mapumzikoni huko Florida anaishi pia katika jengo hilo na ana ofisi pia katika jengo hilo.

Mwandishi: Isaac Gamba/ APE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo