1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amtimua Mkurugenzi wa FBI

Bruce Amani
10 Mei 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amemtimua Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani – FBI, James Comey, hatua ambayo imezusha shutuma kutoka kwa pande zote za kisiasa

https://p.dw.com/p/2cisd
Washington Senat Aussage FBI Director James Comey
Picha: Reuters/K. Lamarque

Utawala wa Trump umesema hatua hiyo imetokana na makosa kadhaa ambayo Comey alifanya katika namna alivyoshughulikia uchunguzi kuhusiana na barua pepe za aliyekuwa waziri wa mambo ya kigeni Hillary Clinton.

Hata hivyo, hatua hiyo imezusha maramoja shutuma za uingiliaji wa kisiasa katika uchunguzi huo wa Urusi, wakati Warepublican na pia Wademokrat wakielezea kusikitishwa kwao.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House imesema Comey aliachishwa kazi kwa kuzingatia mapendekezo ya wazi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu Jeff Sessions na Naibu wake Rod Rosenstein. Rosenstein amekosoa namna Comey alivyoshughulikia kashfa ya barua pepe za Clinton, ikiwa ni pamoja na kukataa mwezi Julai kumfungulia mashitaka na pia matamshi yake ya umma kuhusiana na uchunguzi huo.

Bildkombo James Comey und Hillary Clinton
Comey amekuwa akiendesha uchunguzi kuhusu kashfa ya barua pepe za Hillary ClintonPicha: Getty Images/AFP/Y. Gripas/J. Sullivan

Kwa mujibu wa gazeti la LA Times, tangazo hilo la kumfuta kazi Comey lilimkuta ghafla, na kuwa alifahamu kuhusu kutimuliwa kwake kupitia habari za televisheni wakati alikuwa akizungumza na maafisa wa FBI mjini Los Angeles. Deirdre Fike, ni naibu mkurugenzi wa ofisi ya FBI mjini Los Angeles "Hivyo bila kujali nani anaongoza shirika hili, jukumu letu linabakia lile lile: tupo hapa kuidumisha katiba. Tupo hapa kuwalinda Wamarekani na tunataka kufanya hivyo kadri tunavyoweza na nguvu kazi inayowajumuisha watu kutoka matabaka mbalimbali.

Richard Burr, mwenyekiti wa chama cha Republican wa Kamati ya Ujasusi katika baraza la Seneti amesema amepata wasiwasi kuhusiana na muda na sababu ambazo zimetolewa kwa kutimuliwa Comey. Seneta John McCain amesema hatua hiyo imethibitisha "haja ya kamati maalum ya bunge kuchunguza kwa haraka uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi wa mwaka wa 2016.

Wapinzani Wademocrat pia walikosoa muda ambao hatua ya kumfuta kazi Comey imechukuliwa. Kiongozi wa upinzani katika baraza la Seneti Chuck Schumer amesema kama utawala wa Trump ulikuwa na vipingamizi kuhusu namna mkurugenzi wa FBI Comey alishughulikia uchunguzi wa Clinton, walikuwa na vipingamizi hivyo wakati tu rais alipoingia madarakani. Lakini hawakumfuta kazi wakati huo. Hii ni sehemu ya mwenendo unaotia wasiwasi kutoka kwa utawala wa Trump. Walimtimua Sally Yates, wakamtimua Preet Bharara, na sasa wamemtimua Mkurugenzi Comey, mtu ambaye anaongoza uchunguzi wenyewe. hii haionekani kuwa sadifa. Uchunguzi huu unapaswa kuangaliwa kwa makini kuanzia White House, na kufika mbali kabisa iwezekanavyo kutoka kwa mtu yoyote ambaye Rais Trump amemteua

Wakati huo huo, atakutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, ikiwa ni mkutano wa kwanza ana kwa ana na kiongozi wa ngazi ya juu wa Urusi tangu rais huyo alipoingia madarakani. Itaashiria kuwa nchi hizo mbili zimeimarisha mahusiano yao ambayo Trump hivi karibuni aliyaelezea kuwa katika kiwango cha chini kabisa.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP
Mhariri: Caro Robi