1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aomba radhi kwa matamshi ya kuwakosea adabu wanawake

8 Oktoba 2016

Trump aomba radhi kwa lugha chafu

https://p.dw.com/p/2R2ZK
USA Donald Trump entschuldigt sich für sexistische Aussagen
Picha: REUTERS

Trump aliomba radhi Jumamosi (08.10.2016) kwa kutumia lugha hiyo chafu kuhusu kuwatomasa na kuwabusu wanawake katika mkanda wa video wa mwaka 2005.Kutolewa kwa mkanda huo kumeitibuwa kampeni yake na kusababisha kulaaniwa na wanachama wenzake kutoka chama chake mwenyewe cha kisiasa.

Trump amesema katika taarifa ya video iliowekwa kwenye mtandao wa Twitter "Nimefanya mambo ninayoyajutia.Mtu yoyote anayenifahamu anajuwa kwamba maneno haya hayamaanishi mim ni mtu wa aina gani.

Nimesema nilikuwa sio sahihi na naomba radhi."

Wanachama wenzake wa chama cha Republikan wamelaani lugha aliyoitumia mgombea huyo.Spika wa Baraza la Wawakilishi Paul Ryan afisa mwandamizi wa chama hicho amesema "amechafuliwa " na matamshi hayo na amefuta tukio la kampeni lililokuwa lifanyike Wisconsin pamoja na Trump hapo Jumamosi.

Wanachama wenzake wamuacha mkono

USA Sprecher des Repräsentantenhauses Paul Ryan
Spika wa Baraza la Wawakilishi la bunge la Marekani Paul Ryan.Picha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Reince Preibus mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Chama cha Republikan amesema "Mwanamke yoyote hapaswi aelezewe kwa maneno hayo au kuzungumziwa kwa njia hiyo. Kamwe!"

Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa chama cha Republikan Jason Chaffetz wa Utah ambaye ni mmojawapo wa mkosoaji mkubwa wa Clinton amesema ametenguwa kumuidhinisha Trump akikiambia kituo cha televisheni cha CNN kwamba angelishindwa kumuangalia usoni mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 15.

Mbunge wa Republikan Mike Coffman kutoka Colorado amekiambia kituo cha televisheni cha CBS kwamba Trump anapaswa akae kando na kwamba kushindwa kwake kufikia hatua hii inaonekana kuwa ni  jambo la uhakika.

Kauli hiyo imepelekea kuomba radhi hadharani kwa mara ya kwanza na Trump katika kampeni yake ya kuwania urais iliojaa matusi na kauli za kiburi.Katika ukanda huo wa video wa mwaka 2005 tajiri huyo aliyekuja kwa nyota wa vipindi vya televisheni alisikika akitumia lugha ya kudunisha wakati akimtongoza mwanamke aliyeolewa na kutomasa wanawake.

Amesema"Wakati unapokuwa nyota wanakuachia ufanye hayo.Unaweza kufanya chochote kile."

Mkanda watolewa wakati mbaya

USA Republikaner Wahlkampf Donald Trump in Reno, Nevada
Donald Trump.Picha: Reuters/M. Segar

Mkanda huo wa video ulirekodiwa na kipindi cha televisheni cha "Accesss Hollyood " wakati akiwa safarini ndani ya basi kwenda kurekodi sehemu ya igizo la "Days of Our Lives".

Mkanda huo wa video umetolewa ikiwa imebakia siku moja kabla ya kufanyika kwa madahalo wa pili baina ya wagombea urais Trump na Hilary Clinton hapo Jumapili usiku(09.10.2016) ambao unaonekana ni muhimu kwa Trump kujaribu kurudi tena kwenye umashuhuri baada ya uchunguzi wa maoni kuonyesha amefanya vibaya katika madahalo wa kwanza.

Amesema jambo hilo ni kutaka kuleta ubabaifu ili watu wasizingatie yale muhimu inayoyakabili Marekani leo hii.Amesema ataufunga mjadala wake wa kuwania urais kwa hoja kwamba mpinzani wake Clinton amefanya dhambi kubwa dhidi ya wanawake na pia kugusia uzinzi wa mume wake rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton.

Amesema watayajadili hayo zaidi siku zinazokuja.Wakutane naye hapo Jumapili.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters/AP/AFP

Mhariri : Yusra Buwayhid