1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asema madai ya ngono ni uwongo mtupu

Bruce Amani
14 Oktoba 2016

Kampeni za kinyang'anyiro cha kuingia Ikulu ya White House zinaendelea kupamba moto nchini Marekani huku kila mgombea akijitahidi kujinadi kwa Wamarekani kwa kumkosoa mpinzani wake

https://p.dw.com/p/2RDLZ
Donald Trump
Picha: Picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Donald Trump amevishutumu vyombo vya habari Marekani kwa kuripoti kile alichokitaja kuwa "uwongo mtupu” kuwa aliwadhalilisha wanawake kingono, wakati mke wa rais, Michelle Obama akimshambulia kwa ujumbe mkali mgombea huyo wa Republican. 

Zikiwa zimesalia siku 25 kabla ya wapiga kura nchini Marekani kumchagua mrithi wa mumewe mnamo Novemba 8, Michelle Obama aliyeonekana mwenye hasira alitoa hotuba kali na kumshambulia mfanyabiashara bilionea Trump akiilaani "tabia yake ya kufedhehesha”. Ameuambia mkutano wa kumpigia debe mgombea wa Democratic Hillary Clinton mjini New Hampshire kuwa ni wakati wa kumkomesha Trump. "Haijalishi uko chama gani, Democratic, Republican, au asiye na chama. Hakuna mwanamke anayestahili kufanyiwa hivi, aina hii ya dhuluma. Nafahamu hii ni kampeni, lakini hili halihusu siasa, ni kuhusu maadili ya ubinaadamu, ni kuhusu kizuri na kibaya na hatuwezi kuendelea kuvumilia hilo au kuwaweka watoto wetu katika hali hii sio tu dakika moja bali miaka minne ijayo. Ni wakati wa sisi sote kusimama na kusema inatosha sasa". Alisema Bi Obama.

Michelle Obama amemshutumu Trump kwa kuwafedhehesha wanawake
Michelle Obama amemshutumu Trump kwa kuwafedhehesha wanawakePicha: Picture-Alliance/AP Photo/J. Cole

Mumewe, kisha baadaye akaongeza joto alipotua katika jimbo muhimu la Ohio akiwashambulia Warepublican kuhusiana na meli yao inayozama. Obama amesema Trump alitoka kwenye "dimbwi la kichaa” ambalo lilitengenezwa na Warepublicans kwa miongo mingi. "Wanafahamu vyema. Wengi wa watu hawa waligombea na hawakusema chochote. Na hivyo hawastahili pongezi kwa hilo, katika dakika ya mwisho, wakati mtu waliyemteua na kumuidhinisha na kumuunga mkono ananaswa kwenye mkanda akisema mambo ambayo mtu mwenye maadili hangeweza kufikiria na kusema, na kujisifu, na kucheka au kufanyia mzaha na kuyachukulia hatua". Alisema Obama.

Lakini Trump mwenye umri wa miaka 70 alisimama kidete, akiwakemea wakosoaji wake kuwa ni "waongo wakubwa” na kumshtumu Bi Clinton kwa kula njama na vyombo vya habari ili kuhujumu kampeni yake. Karibu wanawake sita wametuhumu Trump kwa kujaribu kuwapapasa na kuwabusu kwa lazima katika matukio yaliyoripotiwa na New York Times, NBC, People Magazine na mengine, baada ya Mrepublican huyo kusema katika mdahalo wa Jumapili iliyopita na Bi Clinton kuwa hakuwahi kumdhalilisha mwanamke kingono. Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo la West Palm Beach, Trump alisema "Nilitoa hotuba mapema leo kuhusu uwongo huu, ufisadi na tuhuma za uwongo za kampeni ya Hillary mpotovu na vyombo vya habari, ambavyo wanavidhibiti sawasawa. Wanataka tusahau kuhusu Wikileaks. Ufichuzi wa Wikileaks unafurahisha. Wanataka tusiongelee masuala haya". 

Wakati huo huo Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa habari – CPJ imesema kuwa Trump ni tishio kwa uhuru wa habari. Kundi hilo limesema haliegemei upande wowote katika uchaguzi wa Marekani, lakini unatambua kuwa urais wa Trump unaweka kitisho katika uhuru wa habari katika historia ya kisasa

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga