1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump avishambulia vyombo vya habari

Sylvia Mwehozi
12 Januari 2017

Rais Mteule wa Marekani Donald Trump amefanya mkutano wa kwanza na waandishi wa habari na kuelezea masuala kadhaa juu ya mahusiano yake na Urusi, udhibiti wa kampuni zake, na ujenzi wa ukuta na Mexico.

https://p.dw.com/p/2VgAo
New York City Trump erste PK als designierter Präsident
Picha: Getty Images/AFP/T. A. Clary

Trump ameonekana kukubali kwamba Urusi ilihusika na udukuzi wa uchaguzi mkuu lakini akisema mataifa mengine pia yamewahi kuingilia uchaguzi wa taifa hilo. 

Akijibu maswali kadhaa katika mkutano wake wa kwanza na vyombo vya habari tangu achaguliwe, Trump amesema anaamini ni faida kwa Marekani ikiwa mataifa hayo mawili yataelewana, akisema huo ni "mtaji" wala sio "deni" kwa sababu kumekuwa na mahusiano mabaya baina ya mataifa hayo mawili.

"Kuhusu suala la udukuzi sasa nafikiria Urusi ilihusika. Lakini tumedukuliwa na nchi nyingi pamoja na watu wengine na ninaweza kusema unajua , wakati tulipopoteza majina ya watu milioni 22 na kila kitu kilichodukuliwa hivi karibuni, hakuna aliyesema kitu , jambo ambalo lilikuwa kubwa, huenda ilikuwa China. Tuna udukuzi mwingi unaoendelea."

Mashirika ya kijasusi

James Clapper
Mkurugenzi wa ujasusi wa taifa James Clapper Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Scott Applewhite

Trump pia amekiri kuwa ni "udhalilishaji" kwa mashirika ya kijasusi ya Marekani kuruhusu ripoti zilizovuja katika vyombo vya habari ambazo hazikuthibitishwa , zinazodai kwamba Urusi ilikusanya taarifa zinazomhusu yeye ambazo ingezitumia kutaka kumlagai ili kufichua siri zake. Urusi imekanusha madai hayo huku msemaji wa Rais wa Urusi Dmitry Peskov, akiwaeleza waandishi wa habari kuwa ikulu ya Urusi haina taarifa zozote zinazoweza kutumiwa dhidi ya Trump.

Naye Mkurugenzi wa ujasusi wa taifa James Clapper amesema amezungumza na Trump kuhusu taarifa hizo zilizovuja akisema haamini ikiwa jumuiya za kijasusi za Marekani zilivujisha nyaraka hizo katika vyombo vya habari.

Mahusiano na vyombo vya habari

Katika mkutano huo na wanahabari uliochukua saa moja rais mteule Trump ameonekana kujawa na hasira na kuvishambulia baadhi ya vyombo hivyo kikiwemo kituo cha utangazaji cha CNN kuwa ni chombo cha "habari za uwongo" na kukataa kujibu maswali ya waandishi wake. Trump alibishana na mwandishi Jim Acosta wa CNN na amenukuliwa akisema, "hapana sio wewe, sio wewe, shirika lako ni la hovyo! kaa kimya! nyamaza, siwezi kukupa nafasi ya kuuliza swali nyie ni chombo cha habari za uwongo."

USA Befragung Senat - Rex Tillerson, designierter Außenminister
Rex Tillerson mteule wa Trump kuwa waziri wa mambo ya nje Picha: Reuters/J. Ernst

Wakati wa mkutano huo Trump pia ametangaza kuachia udhibiti wa kampuni zake kwa watoto wake wakubwa Donald Trump Jr. na Eric Trump.

Lakini wakati hayo yakijiri mteule wa rais huyo katika nafasi ya waziri wa mambo ya kigeni Rex Tillerson ameonyesha kutofautiana na bosi wake katika baadhi ya mambo ikiwemo mahusiano na Urusi ambayo amesema ni "hatari", wakati alipohojiwa na kamati ya masuala ya kigeni ya seneti. "Ni lazima pia tuwe macho kuhusu mahusiano yetu na Urusi . Urusi leo inaleta hatari kubwa lakini haitabiriki katika kuendeleleza maslahi yake binafsi. Imeivamia Ukraine. ikiwemo kuichukua Crimea na kuviunga mkono vikosi vya Syria na kukiuka sheria ya vita."

Kuhusu ujenzi wa ukuta wa Mexico kiongozi huyo amesema ahadi yake iko palepale akisema Marekani itafadhili upande wa mbele wakati Mexico ikigharamia ujenzi wake. Muda mchache baadae rais Enirique Pena Nieto wa Mexico amejibu kwa kukataa mahitaji hayo ya Trump.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters

Mhariri: Lilian Mtono