1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump awashambulia wahamiaji kwa mara nyengine

Yusra Buwayhid1 Septemba 2016

Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump, akiwa anahutubia katika jimbo la Arizona ameapa kuwa atakapoingia ikulu baada ya uchaguzi ujao, kila aliyeingia Marekani kinyume na sheria atarejeshwa kwao.

https://p.dw.com/p/1JtQ0
USA Donald Trump hält eine Rede in Phoenix
Picha: Reuters/C. Allegri

Sera ya Trump ya uhamiaji anayoitangaza kwa kutumia lugha isiyo ya kidiplomasia, imekuwa ikiwakera wengi wakiwamo raia wa Mexico, nchi aliyoizuru kwa mara ya kwanza hapo jana kama mgombea urais wa Marekani.

Katika hotuba yake jimboni Arizona, Trump amewashambulia watu milioni 11 walioingia Marekani kinyume na sheria, wiki moja baada ya kuwataja kwa wema na kuwasifu kwa mchango wao wa miaka kadhaa katika jamii ya watu wa Marekani.

Katika hotuba yake hiyo, Trump amesisitiza kuwa atakapoingia ikulu, suala la kuwafukuza wahamiaji walioshitakiwa kwa makosa ya kihalifu atalipa kipaumbele.

"Nitaanzisha kikosi maalumu cha kuwafukuza wahamiaji nchini. Kazi yake kuu itakuwa ni kuwasaka na kuwarejesha walipotoka wahamiaji wahalifu walioingia Marekani kwa kukwepa sheria za nchi, kama alivyozikwepa sheria Hillary Clinton, pengine naye watamfukuza," amesema Donald Trump.

Trump amesema iwapo atashinda katika uchaguzi ujao wa Novemba 8, basi watu wote walioingia Mreakani kinyume na sheria watakuwa na njia moja tu ya kutambulika kisheria nchini humo: Kurudi nyumbani walipotoka, na kuomba tena ruhusa ya kuingia nchini humo.

USA Mexiko Donald Trump Besuch Pressekonferenz
Mgombea urais kwa tiketi ya Rebublican, Donald Trump, akiwa na rais wa Mexico, Pena Nieto.Picha: Reuters/H. Romero

Ameongeza kuwa ujumbe wake kwa ulimwengu mzima ni kwamba haiwezekani kupata uraia wa Marekani kwa kuingia nchini humo kinyume na sheria.

Wamexico wakasirishwa na Nieto

Trump kwa mara nyengine amerudia kauli yake ya kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico. Ameyasema hayo masaa machache baada ya kuzungumza uso kwa macho na rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto, ambaye alimwambia wazi Trump kuwa nchi yake haitolipia ujenzi wa ukuta huo.

Hapo jana wakiwa katika mkutano na waandishi habari nchini Mexico, Trump alidai kwamba yeye na Nieto hawakulizungumzia suala la nani atalipia ujenzi wa ukuta huo. Nieto alibaki kimya kwa wakati huo.

Lakini, katika ukurasa wake wa Twitter Nieto amesema katika mazungumzo ya faragha na Trump amemueleza waziwazi kuwa nchi yake haitobeba jukumu hilo la kulipia ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico.

Kitendo cha kiongozi huyo wa Mexico kubaki kimya huku Trump akipaza sauti kuwa atajenga ukuta baina ya nchi hizo mbili kimewakasirisha sana raia wa Mexico. Nieto alishambuliwa vikali na raia wake katika mitandao ya kijamii wanaokikiangali kitendo cha kumkaribisha Trump kama udhalilishaji wa kitaifa. Katika kampeni zake mwanasiasa huyo amekuwa akiwataja wahamiaji wa Mexico kuwa ni wahalifu na wabakaji.

Mbali na hilo, Wamexico pia wamekasirishwa na Rais wao kwa kushindwa kumtaka Trump aoembe msamaha kwa kuwaita Wamexico wanaoishi Marekani kuwa ni wahalifu na wabakaji.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ape

Mhariri:Iddi Ssessanga