1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Clinton wakabiliana katika mdahalo

Bruce Amani
27 Septemba 2016

Wagombea wa urais Marekani Donald Trump na Hillary Clinton wamekabiliana kuhusu ajenda zao katika mdahalo wa kwanza ambao kila mmoja alimshambulia mwenzake na uliojaa mivutano

https://p.dw.com/p/2Qcv9
USA Wahlkampf TV Duell
Picha: Getty Images/DW Montage

Mdahalo huo uliosubiriwa kwa hamu uliangazia sera za kiuchumi za wagombea hao wawili, mahusiano ya jamii, vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu na mahusiano ya kimataifa ya Marekani.

Mrepublican Trump alionekana mwenye ujasiri mwanzoni wakati akionyesha upinzani wake kwa mikataba ya kibiashara, akijadili maoni yake kuhusu mahusiano ya jamii na kupigana na uhalifu. Wakati mdahalo uligeukia sera ya kigeni, Mdemocrat Clinton alichukua usukani na kuonekana kumwekea chambo Trump licha ya juhudi zake za mara kwa mara za kuingilia kati..Katika uchunguzi wa haraka uliofanywa na televisheni ya CNN kwa kuwashirikisha wapiga kura 521, asilimia 62 walisema Clinton alishinda mdahalo huo dhidi ya asilimia 27 ya Trump.

USA Wahlkampf TV Duell
Trump na Clinton walisalimiana kwa kupeana mikono na tabasamu kabla ya kuanza mdahaloPicha: Reuters/L. Jackson

Mdahalo huo wa kwanza kati ya mitatu umekuja wakati kinyang'anyiro cha urais kianza kuwa kikali. Matokeo ya uchunguzi wa maoni yaliyotolewa Jumatatu yalionesha ushindani mkali katika kiwango cha kitaifa, ambapo wagombea wote walipata asilimia 46 katika uchunguzi wa shirika la Bloomberg.

Kila mgombea alijaribu kumwelezea mwenzake kuwa asiyefaa kuongoza Marekani. Majadiliano yalihusu masuala kadhaa tata kuanzia uamuzi wa Trump kutotangaza maelezo ya mapato na matumizi hadi kwa uamuzi wa Clinton kutumia anuani ya kibinafsi ya barua pepe wakati akiwa waziri wa mambo ya kigeni na Trump kueneza uwongo kuwa Rais Barack Obama hakuzaliwa Marekani. "huenda hataki Wamarekani - nyote mnaotazama usiku huu - kujua kuwa hajalipa kodi yoyote kwa serikali kwa sababu miaka pekee ambayo mtu aliwahi kuona hilo ni miaka kadhaa iliyopita alipolipa kodi wakati akijaribu kutafuta leseni ya biashara ya kamari na mamlaka zikaonyesha hakulipa kodi yoyote kwa serikali.." alisema Clinton.

Trump alisema ataweza tu kutoa maelezo ya mapato ya kodi na matumizi yake kama Clinton atatoa maelfu ya barua pepe alizofuta "Nitatoa maelezo yangu kuhusu kodi kinyume na matamanio ya mawakili wangu, wakati Clinton atatoa barua pepe 33,000 ambazo zilifutwa. Mara tu atapozitoa, nitatoa maelezo yangu ya mapato na itakuwa kinyume cha ushauri wa mawakili wangu, wanaoniambia nisitoe usitoe" alijibu Trump

USA Wahlkampf TV Debatte Trump Clinton Hofstra
Mdahalo wa urais ulitazamwa na karibu Wamarekani milioni 100Picha: Reuters/S. Stapleton

Trump alimkosoa Clinton kwa kuunga mkono mikataba ya biashara isiyokuwa na tija akitoa mfano wa Makubaliano ya Biashara Huru kati ya Marekani na Canada na Mexico yaliyosainiwa na mumewe aliyekuwa rais Bill Clinton.

Aidha walikabiliana kuhusu suala la mahusiano ya jamii kwa kujadili marekebisho ya mfumo wa sheria ya kuwashtaki wahalifu, ambayo Clinton alisema anaunga mkono ili kurejesha imani baina ya jamii na polisi.

Wakati mdahalo uligeukia masuala ya kimataifa, waziri huyo wa zamani wa mambo ya kigeni wa Marekani aliahidi kuwasaidia washirika wa Marekani, naye Trump akasema Marekani haipaswi kubeba mzigo wa mahitaji ya ulinzi duniani akiongeza kuwa nchi kama vile Ujerumani na Japan zinapaswa kulipia sehemu yao. Clinton aliishutumu Urusi kwa udukuzi wa karibuni wa data za mtandao wa intaneti katika ofisi za kampeni za Democratic. Trump anayeshutumiwa kuwa na mahusiano ya karibu na Urusi alisema huenda ikawa ni Urusi lakini pia China.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Gakuba Daniel