1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Clinton wazidi kutamba katika chaguzi za mchujo

Caro Robi27 Aprili 2016

Donald Trump ameshinda katika majimbo yote matano ya kaskazini mashariki katika uchaguzi wa mchujo jana na hivyo kuendelea kuwa na nafasi nzuri zaidi dhidi ya wapinzani wake kupata tiketi ya chama cha Republican.

https://p.dw.com/p/1IdEn
Picha: Getty Images/AFP/E. Munoz Alvarez/S. Platt

Trump aliwabwaga vibaya wapinzani wake Ted Cruz na John Kasich kwa kupata ushindi wa kishindo katika majimbo ya Maryland, Deleware, Pennsylvania, Rhode Island na Connecticut.

Licha ya kuwa vigogo wa chama cha Republican wana mashaka naye na wapinzani wake wawili wameungana ili kumzuwia asije akapata idadi ya wajumbe wanaohitajika kushinda tiketi ya kupeperusha bendera ya Republican, kwa mara nyingine Trump amedhihirisha kupendwa miongoni mwa wajumbe wa Republican.

Clinton kifua mbele kwa upande wa Democrats

Baada ya ushindi huo, mfanyabiashara huyo bilionea amesema kufikia sasa hana shaka yeye ndiye mgombea mteule wa Republican. Kwa upande wa chama cha Democrats, Hillary Clinton alishinda katika majimbo manne, isipokuwa katika jimbo la Rhode Island ambapo Bernie Sanders alishinda.

Wagombea urais Marekani Hillary Clinton na Donald Trump
Wagombea urais Marekani Hillary Clinton na Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa/Skidmore/

Akiwahutubia wafuasi wake mjini Philadelphia katika jimbo la Pennsylvania, Bi Clinton ameutaja usiku wa Jumanne kuwa usiku mzuri sana.

Trump mwenye umri wa miaka 69 amepata kura zaidi ya asilimia 50 kwa majimbo yote matano na hivyo kusalia mstari wa mbele kueleka kupata wajumbe 1,237 wanaohitajika kabla ya mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama utakaofanyika mwezi Julai.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa James Morone amesema kwa wiki kadhaa wanaompinga Trump wamekuwa wakinadi kampeini ya kutaka kumzuia kushinda uteuzi wa chama lakini matokeo ya majimbo hayo matano yanaonyesha kuwa kampeini hiyo haikusaidia kitu.

Cruz na Kasich watapatapa

Ushindi wa Bi Clinton, waziri wa zamani wa mambo ya nje na mke wa Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton unazidi kumshinikiza Sanders kujiondoa kutoka kinyang'ayiro cha urais lakini seneta huyo wa jimbo la Vermont amesema habanduki hadi uchaguzi wa mwisho wa majimbo utakapofanyika katika jimbo la California tarehe 7 mwezi Juni.

Wagombea Urais waRepublican Trump, Cruz na Kasich
Wagombea Urais waRepublican Trump, Cruz na KasichPicha: picture-alliance/AP Photo/P.Sancya

Clinton anatumai kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini Marekani.

Kufikia sasa Trump amepata wajumbe 988, Cruz ana wajumbe 568 na Kasich ana wajumbe 152. Sasa macho yanaelekezwa katika jimbo la Indiana ambako Cruz ana matumaini atashinda katika uchaguzi wa taraehe tatu mwezi ujao. Majimbo matano ndiyo yamesalia kupiga kura katika chaguzi za mchujo za vyama yakiwemo majimbo ya Indiana, New mexico, Oregon na California.

Morone anasema iwapo Trump atashinda Indiana itakuwa vigumu mno kumzuia kuchukua tiketi ya Republican ya kugombea urais. Uchaguzi wa Rais nchini Marekani unatarajiwa mwezi Novemba.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Hamidou Oummilkheir