1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Putin wasema nguvu za kijeshi sio suluhisho Syria

Caro Robi
11 Novemba 2017

Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wamekubaliana kuwa mzozo wa Syria hauwezi kumalizwa kwa nguvu za kijeshi bali kisiasa.

https://p.dw.com/p/2nSYh
APEC Donald Trump und Wladimir Putin
Picha: Getty Images/M.Klimentyev

Viongozi hao walitoa tamko la pamoja pembezoni mwa Mkutano mkuu wa viongozi wa jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Asia na Pacifiki (APEC) katika mji wa Da nang nchini Vietnam. Trump na Putin pia wameeleza kwamba watashirikiana katika juhudi za kupambana na kundi la wanamgambo wenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu IS.

Walizungumza baada kuwepo tashwishi hapo awali kama viongozi hao wangelikutana. Taarifa kutoka Ikulu ya Rais wa Urusi zimesema tamko la marais hao limeonyesha kuridhika kwa viongozi hao kutokana na juhudi za kuzuia mivutano baina ya majeshi yao yaliyoko nchini Syria.

Jeshi la Urusi hivi karibuni limekuwa likiilaumu Marekani kwa kujifanya inapambana na IS nchini Irak na pia kwa kuizuia operesheni inayoungwa mkono na Urusi mashariki mwa Syria.

Trump na Putin wazungumzia uchaguzi wa Marekani 2016 

Kwa upande mwingine, Trump amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin amemwambia kuwa hakuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka ambao matokeo yake yalipelekea yeye kuingia madarakani.

Vietnam Apec-Gipfel US-Präsident Donald Trump und Wladimir Putin
Rais wa Urusi(Kushoto) Vladimir Putin na wa Marekani Donald TrumpPicha: Getty Images/AFP/J. Silva

Kiongozi huyo wa Marekani amewaambia wanahabari kuwa kila mara Putin anapokutana naye humueleza kuwa hakuingilia uchaguzi wa Marekani na anaamini kile anachomwambia kuwa ukweli.

Uhusiano wa Trump na Urusi umekuwa gumzo katika mwaka wake wa kwanza tangu aingie madarakani huku baadhi ya wasaidizi wake wakifanyiwa uchunguzi kwa madai ya kushirikiana na Urusi.

Rais wa Urusi amemtaja Trump kuwa mtu mwenye heshima na rahisi kutangamana naye akiongeza kuwa hawafahamiani sana lakini amepata taswira kuwa Rais Trump ni mtu muungwana na mcheshi.

Alipoulizwa na wanahabari kuhusu madai nchi yake iliingilia uchaguzi wa Marekani, Putin amesema hizo ni ndoto tu zilizo na lengo la kuhujumu utawala wa Trump.

Baada ya kutilia msisitizo mwaka jana wakati wa kampeini za uchaguzi wa Rais, Trump alisema litakuwa jambo jema iwapo Urusi na Marekani ziatshirikiana kuyatatua matatizo ya ulimwengu, viongozi hao wawili hawajaonekana kukutana mara kwa mara tangu Trump kuingia madarakani.

Trump Jumamosi ameuzuru mji mku wa Vietnam, Hanoi, kituo chae cha kumi katika ziara ya siku 11 barani Asia. Baada ya hapo anatarajiwa kuizuru Ufilipino Jumapili ambako atakutana na mwenyeji wake Rais Rodrigo Duterte.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/afp/dpa

Mhariri: Zainab Aziz