1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump na Ukuta na Reichsbürger Magazetini

Oumilkheir Hamidou
26 Januari 2017

Trump na ujenzi wa ukuta, kuchaguliwa Martin Schulz kugombea kiti cha kansela kwa tikiti ya chama cha Social Democratic na kundi hatari la wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wasiotaka kuheshimu sheria Magazetini

https://p.dw.com/p/2WQL0
Symbolbild Reichsbürger
Picha: picture-alliance/dpa

Tunaanzia Marekani lakini ambapo rais mpya Donald Trump anaendelea kugonga vichwa vya habari. Ahadi alizotoa katika kampeni za uchaguzi anaanza kuzitekeleza. Mojawapo ya ahadi hizo ni kuzungusha mpaka unaoigawa Marekani na Mexico. Gazeti la "Badische Zeitung"linachunguza maoni ya wananchi wa Marekani kuhusu ukuta huo na kuandika: "Wananchi wengi wa Marekani wanauangalia mpango wa ujenzi huo wa ukuta kwa jicho la wasi wasi-na wana kila sababu ya kuwa hivyo. Katika ukuta huo wenye urefu mara dufu wa ule uliokuwa ukiigawa zamani Ujerumani, rais Trump anataka kuweka wanajeshi laki moja ili kuwazuwia wahamiaji  wanaotokea kusini. Suala lakini wanalojiuliza ni jee nani atakubali kukata majani ya bustani za wamarekani kwa malipo duni, nani atawajengea njia zilizoahidiwa, daraja na njia za chini ya ardhi? Kujenga ukuta sio tu ni uamuzi wa kipumbavu, bali pia  ni ghali na si wa kimarekani."

Martin Schulz pekee hatoweza kuibadilisha hali ya mambo

Nchini Ujerumani kitandawili cha nani atagombea kiti cha kansela kwa tikiti ya chama cha Social Democratic SPD uchaguzi  mkuu utakaopitishwa septemba 24 inayokuja kimeshapatiwa jibu. Na  maoni ya wananchi yameshaanza kusikika tangu spika huyo wa zamani wa bunge la Ulaya alipoteuliwa.Hata hivyo gazeti la kusini magharibi, "Stuttgarter Nachrichten" linaandika: "Si ajabu kuwaona wanasiasa wa CDU/CSU wakifuatilizia kwa makini, lakini bila ya pupa, umuzi wa nani atagombea kiti cha kansela. Ni kweli kwamba Schulz ana nafasi kubwa ya kushughulikia kampeni za uchaguzi kwasababu halazimiki kufuata mwongozo wowote wa serikali ya muungano. Hata hivyo Merkel halazimiki kujibadilisha ili aweze kumshinda Schulz. Spika huyo wa zamani wa Bunge la ulaya ingawa ni mashuhuri kuliko Sigmar Gabriel, hata hivyo si kitisho kwa kansela. Schulz ni mwana SPD aliyebobea. Lakini SPD wanabidi wawe wa kweli: wasimtupie Gabriel pekee makosa ya kuporomoka hadhi yao hadi kusalia asili mia 20. Mgombea naawe mchangamfu vipi, hatoweza peke yake kuufanya uongozi uaminike. Schulz ni mapambazuko lakini bado si mkombozi.

Kitisho kwa maisha ya jamii kinachotokea kulia

Nchini Ujerumani limeibuka kundi la "wahalifu" wasiotaka kuheshimu sheria wala kanuni-wenyewe wanajiita "Reichsbürger" kwa kiswahili tunaweza kuwaita "Raia wa enzi za Raish". Kundi hilo la siasa kali za mrengo wa kulia linachunguzwa na idara za upelelezi nchini Ujerumani. Gazeti la Donaukurier linaandika: "Tangu Novemba kundi hilo dogo linachunguzwa mtindo mmoja na idara za upelelezi. Kilichotokana na uchunguzi huo kinatisha: Pekee katika jimbo la kusini la Bavaria kuna wafuasi zaidi ya 340 wa kundi la Reichsbürger wenye silaha. Na hivi karibuni, watuhumiwa wawili wanaosemekana kuwa wafuasi wa kundi hilo wanasemekana wamebuni kundi la kigaidi na kuandaa mipango ya kufanya mashambulio. Kukamatwa kwao kunabainisha kwamba mjadala kuhusu usalama wa ndani nchini Ujerumani utahodhi kampeni za uchaguzi mkuu. Na  mwenye kuwamulika pekee watuhumiwa wa kigaidi  makundi ya  itikadi kali ya dini ya kiislam, atakosa kuiona hatari ya siasa kali za mrengo wa kulia.

 

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman