1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: sheria ya uchaguzi imekiukwa Marekani

Zainab Aziz
28 Novemba 2016

Rais mteule Donald Trump wa Marekani anadai kuwa takriban watu milioni 2 walipiga kura kinyume cha sheria. Hayo ni baada ya uwezekano wa kuhesabiwa kura upya katika jimbo la Wisconsin

https://p.dw.com/p/2TMPd
USA Wahlkampf TV Duell
Picha: Getty Images/DW Montage

Ushindi wa rais mteule wa Marekani Donald Trump ulikuwa wa kushangaza hasa ikizingatiwa kuwa mpinzani wake Hilary Clinton alimshinda rais huyo mteule kwa kura milioni 2.2 zaidi za wananchi lakini wajumbe maalum walimwezesha Trump kutwaa ushindi baada ya kumpa kura nyingi kuliko Clinton.  Hata hivyo Trump amedai kwamba angemshinda Clinton kwa wingi wa kura za wananchi, iwapo wapiga kura milioni 2 ambao si wa halali, wasingepewa nafasi ya kupiga kura.  Hayo yanajitokeza baada ya aliyekuwa mgombea katika kinyag'anyiro hicho cha Urais Dr. Jill Stein wa chama cha Kijani kuwasilisha hati ya kuhesabiwa upya kura katika jimbo la Wisconsin ambalo Trump alishinda.  Upande wa Hilary Clinton pia unaazimia kuungana pamoja na mgombea huyo wa chama cha Kijani katika zoezi hilo la kuhesabiwa kura upya, ingawa tangu mwanzo Clinton alishasema kuwa haoni ishara zozote za kukiukwa sheria katika kinyang'anyiro hicho cha kuingia ikulu ya White House.  

USA Donald Trump
Rais mteule wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/C. Allegri

Trump na wasaidizi wake wanajaribu kupinga uamuzi huo. Msaidizi wa Trump mwenye usemi mkubwa Kellyanne Conway amesema iwapo timu ya Hillary Clinton itaendelea kushinikiza azma ya kutaka kushiriki katika zoezi la kuhesabiwa kura upya katika jimbo la Wisconsin basi kwa upande wake Rais mteule Donald Trump hatasita kufikiria upya juu ya ahadi aliyoitoa kwamba hatamchukulia hatua Clinton kutokana na kutumia e mail yake binafsi wakati alipokuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani.

Wakili wa maswala ya uchaguzi kwa upande wa chama cha Demoktars Marc Erik amesema kwamba kampeni hizo zitaendelea kufanyika kwa ajili ya kuwezesha zoezi la kuhesabiwa kura upya katika majimbo mengine mawili ya Michigan na Pennsylvania.

Wataalamu wa maswala ya uchaguzi wanasema kutokana na matokeo ya jumla katika uchaguzi wa urais uliomalizika nchini Marekani, Clinton alikuwa nyuma ya Trump kwenye majimbo mengi na kwa ajili hiyo itakuwa vigumu kuubatilisha ushindi wa Donald Traump.  

Mwandishi Zainab Aziz/AFPE/DPAE
Mhariri: Yusuf Saumu