1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsvangirai akamatwa tena

29 Machi 2007

Wakati viongozi wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC wakikutana nchini Tanzania juu ya Zimbabwe, polisi wamevamia ofisi za makao makuu ya chama cha upinzani mjini Harare na kumkamata kiongozi wake Morgan Tsvangirai

https://p.dw.com/p/CHHF

Polisi wa kukabiliana na fujo waliokuwa na silaha walizivamia ofisi za makao makuu ya chama cha MDC mjini Harare hii leo na kumtia nguvuni bwana Morgan Tsvangirai na wenzake waliokuweko kwenye ofisi hizo.

Chama cha Movement for Demokratic Change MDC kimesema Tsvangirai alikuwa amejiandaa kuwa na mkutano na waandishi habari wakati walipovamia na polisi.

Uvamizi huo hata hivyo unaelekea utaongeza shinikizo kwa viongozi wa Afrika kuutumia mkutano ulioanza leo Tanzania kumkaripia rais Robert Mugabe ambaye amekuwa akikosolewa kwa kuwakandamiza wapinzani nchini mwake kwa miaka 27 ya utawala wake.

Uingereza tayari imeshakosoa kitendo cha leo cha kukamatwa bwana Tsvangirai na wenzake,Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Margeret Beckett ni miongoni mwa waliokikosoa kitendo hicho akisema serikali ya Mugabe inaonekana imeamua kuendelea na uchokozi.

Katika taarifa ya bibi Beckett amemtaka rais Mugabe na utawala wake kuzingatia miito iliyotolewa na jumuiya ya kimataifa pamoja na nchi zilizo jirani yake za Afrika kuacahana na dhuluma dhidi ya wazimbabwe na kuheshimu haki zao.

Ujerumani ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya imetoa kilio chake kwa rais Mugabe na kusema kwamba inawasiwasi mkubwa juu ya tukio hili la kukamatwa tena kwa Morgan Tschangira na wenzake na kutaka kuonana na kiongozi huyo na wapinzani wenzake wengine wakisiasa.

Hali hii inatoa mtihani mkubwa kwa Viongozi wanaohudhuria mkutano maalum wa kilele wa siku mbili wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC huko nchini Tanzania nchi hizo zimekuwa zikilaumiwa kwa kushindwa kuubana utawala wa Mugabe kufuata demokrasia.

Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema pamoja na uvamizi huo mpya dhidi ya wapinzani uliofanywa na utawala wa Mugabe, viongozi wa Kiafrika katika eneo hilo hawawezi kumshutumu hadharani rais Mugabe na kufuata miito iliyotolewa na nchi za magharibi kwamba wachukue msimamo mkali dhidi ya rais huyo wa Zimbabwe.

Wakati wa kukamatwa Tsvangirai na wenzake hii leo rais Mugabe anayetarajiwa kuelekea Tanzania jioni hii alikuwa akihudhuria mkutano wa chama chake tawala cha ZANU PF mkutano ambao umetajwa na vyombo vya habari nchini Zimbabwe kwamba huenda utazungumzia iwapo kimuunge mkono Mugabe katika harakati zake za kutaka kuongeza kipindi chake cha urais licha ya mzozo nchini humo.

Itakumbukwa kwamba rais Mugabe hivi karibuni alipendekeza kuusogeza mbele uchaguzi wa rais hadi mwaka 2010 au kuwania kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha ZANU PF endapo uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa mwaka ujao na akishinda abakie kuwa rais kwa kipindi kingine cha miaka sita.