1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsvangirai ampa saa 24 Mugabe

Hamidou, Oumilkher26 Juni 2008

Viongozi wa Zimbabwe watakiwa wawajibike

https://p.dw.com/p/ERG6
Morgan Tsvangirai akizungumza na waandishi habari mjini HararePicha: AP


Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai amelisihi bara la Afrika liingilie kati katika mzozo wa nchi yake,akimpa wakati huo huo rais Robert Mugabe muda wa saa 24 akubali kujadiliana.



Katika mahojiano pamoja na gazeti la Uengereza "Times",kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC,Morgan Tsvangirai, aliyeamua kususia duru ya pili ya uchaguzi wa rais, amesema halitozuka tena suala la kujadiliana pamoja na Mugabe ikiwa uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa hapo kesho.


 Morgan Tsvangirai anamtaja rais Mugabe kua "ni kiongozi haramu" ."Hakutakua tena na majadiliano ikiwa Mugabe atajitangaza mshindi na kuendelea kujiiita rais,"amesema hayo kiongozi huyo wa upinzani aliyekimbilia katika ubalozi wa Uholanzi tangu jumapili iliyopita.


Morgan Tsvangirai anamtuhumu rais Mugabe kua nyuma ya visa vya matumizi ya nguvu yaliyogharimu  maisha ya raia kadhaa wasiokua na hatia.


"Anaesakwa hasa ni mie" amesema kiongozi huyo wa MDC akijibu suala lini anapanga kuuhama ubalozi wa Uholanzi.


Morgen Tsvangirai aliyemaaloza wa kwanza katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais  amewatolea mwito viongozi wa Umoja wa Afrika na jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC wabuni mkakati wa muda utakaoiauni nchi yake,na kutoa mwito pia watumwe wanajeshi wa kulinda amani nchini humo.Morgen Tsvangirai anasema:


"Daima tumekua tukisema kwamba tatizo la Zimbabwe linabidi lifumbuliwe na bara la Afrika.Kwa hivyo nnautaka Umoja wa Afrika na jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC kwa pamoja,wasimamie mpango ulioshauriwa na Umoja wa mataifa wa kubuniwa kipindi cha mpito.Tunashauri tume ya suluhu ya Umoja wa Afrika,inayowajumuisha viongozi mashuhuri,ibuni kipindi cha mpito kitakachotilia maanani matakwa ya wananchi wa Zimbabwe,kama walivyotamka March 29 iliyopita."


Mzozo wa Zimbabwe unatazamiwa kugubika mkutano wa viongozi 53 wa umoja wa Afrika watakaokutana kuanzia june 30 hadi July mosi huko Charm El Sheikh nchini Misri.


Kwa upande wa kimkoa,Zimbabwe iligubika mkutano wa dharura ulioitishwa jana na kamisheni ya  usalama ya jumuia ya ushirikiano kusini mwa Afrika SADC mjini Mbabane nchini Swaziland.


Mwishoni mwa majadiliano hayo,mfalme Mswati wa Swaziland,rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambae ndie mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Angola Joao Miranda wametoa mwito "uchaguzi wa Zimbabwe uakhirishwe ."


Hata rais mstaafu wa Afrika kusini Mzee Nelson Mandela ameamua kupaza sauti na kukosoa kile anachokiita "uzembe mkubwa" wa viongozi wa Zimbabwe.


Kwa upande wake waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice akiwa ziarani nchini Japan kuhudhuria mkutano wa mataifa tajiri kiviwanda G8, amewasihi viongozi wa Zimbabwe wafikie makubaliano haraka iwezekanavyo kwa kutilia maanani matokeo ya chaguzi zilizotangulia.


Wakati huo huo watu 200,wake kwa waume na watoto,wanaodai kua wahanga wa matumizi ya nguvu nchini Zimbabwe, wamekimbilia katika ubalozi wa Afrika kusini mjini Harare jana usiku.


►◄