1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma ataka matokeo ya uchaguzi yatangazwe.

Mtullya, Abdu Said9 Aprili 2008

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe awataka viongozi wa kusini mwa Afrika wasaidie kuepusha maafa nchini mwake.

https://p.dw.com/p/Demg


Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai amesema leo kuwa  atatumia fursa ya mikutano na viongozi wa kusini mwa afrika kuwataka viongozi hao wasaidie kuepuesha  maafa  nchini Zimbabwe.


Akizungumza katika mahojiano na radio ya Afrika Kusini kiongozi huyo wa chama    cha upinzani MDC ameeleza kuwa halitakuwa jambo la manufaa kwa nchi   za kusini mwa Afrika ikiwa  nchi jirani-itakuwa na mgogoro.

Bwana Tsvangirai ameeleza hayo baada ya mazungumzo yake na rais wa Botswana Ian Khama.

Baada ya kuzitembelea Botswana,na Afrika Kusini  bwana Tsvangirai anatarajiwa pia kufanya  ziara nchini Zambia na Msumbiji.

Wakati  huo huo jumuiya ya kimataifa imeimarisha  shinikizo kutaka matokeo ya  uchaguzi uliofanyika  tarehe 29 mwezi uliopita yatangazwe nchini zimbabwe.

Kiongozi  wa  chama  kinachotawala nchini  Afrika  Kusini ANC  bwana Jacob Zuma amejiunga   na  kampeni ya kutaka  matokeo ya uchaguzi wa Zimabwe  yatangazwe.Lakini  tume  ya uchaguzi imesema  haitatoa  matokeo hayo.

Mwanasheria wa tume hiyo amesema leo kwamba  itakuwa  hatari kwa mahakama kuu kuamrisha kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais.

Mwanasheria  huyo George Chikumbirike amekataa  kusema ni hatua gani  ya matayarisho iliyofikiwa na tume ya  uchaguzi katika kutangaza matokeo.Amesema  habari hizo ni istihaki ya tume ya uchaguzi na itatangaza  itakapokuwa tayari kufanya hivyo.