1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsvangirai azuiliwa tena leo na polisi

Kalyango Siraj6 Juni 2008

Umoja wa Mataifa walaani hatua ya Harare kupiga marufuku asasi za misaada

https://p.dw.com/p/EEw7
Kiongozi wa chama cha upinzani Zimbabwe Movement for Democratic Change na mgombea wa kiti cha urais Morgen Tsvangirai akihutubia umati wa raia wa nchi yake waliko Afrika kusini katika kituo cha polisi cha Alexandra katika mtaa wa the Alexandra karibu na Johanesburg May 22, 2008. Tsvangirai anasemekana amezuiliwa leo Ijumaa 06.06.08 kwa mara nyingine tena na polisi ya Zimbabwe kuhutubia mkutano wa hadhara.Picha: AP

Polisi ya Zimbabwe imemzuilia kiongozi wa upinzani Morgen Tsvangirai kwa mara nyingine tena.

Haya yamekuja wakati serikali ikiwa imesimamisha mashirika ya kimisaada kuendesha shughuli hizo hadi wakati mwingine,hatua ambayo imelaaniwa na Umoja wa Mataifa.

Kuzuiliwa kwa leo kwa kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC ni kwa pili wiki hii.

Msemaji wa chama hicho, Nelson Chamisa,amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa Tsvangirai amezuiliwa tena katika eneo la Umzingwane alipokuwa anajaribu kutaka kuhutubia mkutano wa hadhara.Awali kiongozi huyo alizuiliwa na polisi kuhutubia mkutano nje ya mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Bulawayo.Chama chake cha MDC kinadai kuwa rais Robert Mugabe anajaribu kumvurugia kampeini zake.

Kiongozi huyo anatafuta kura kufuatia duru ya pili ya uchaguzi wa uraisi itakaofanyika Juni 27.

Hadi kuingia mitamboni tulikuwa hatujapata taarifa ya kuwa ikiwa Tsvangirai alikuwa ameachiliwa kutoka kituo kimoja cha polisi aliko pelekwa.

Na hayo yakiarifiwa mgogoro wa Zimbabwe unaonekana umepata sura mpya kufuatia amri ya serikali kupiga marufuku mashirika ya kutoa msaada kuendesha shughuli hadi wakati mwingine.

Baadhi wanasema ni hadi pale uchaguzi wa duru ya pili utakapomalizika.

Serikali ya Mugabe inayalaaumu baadhi ya mashirika kwa kujiingiza katika masuala ya kisiasa.

Umoja wa Mataifa kwa upande wake umeonya kuwa shughuli zake za kimisaada nchini humo zitaathirika mno na agizo la serikali.

Msemaji wa ofisi ya shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia misaada ya kibinadamu, Elisabeth Byrs,amesema kuwa ni wananchi ndio watakaoteseka na hatua hiyo ya serikali ikiwa shughuli za kimisaada zitavurugika.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unataraji kuwa mashirika hayo yataruhusiwa tena kufanya kazi,huku akisema mashirika hayo ni muhimu sana kwa shughuli zake kwani ni washirika wakuu wa kazi zake.

Pia ametetea mashirika hayo akisema yanafuata muongozo tu unaohusiana na misaada ya kibinadamu.

Serikali ya Zimbabwe, ikitoa sababu za kujihusisha katika masuala ya kisiasa,imesema kuwa shirika lolote linalotaka kufanya kazi nchini humo ni lazima lijiandikishe upya ili kuweza kupewa kibali cha kufanya kazi na pia shirika hilo liahidi kuwa halitajihushisha katika siasa za ndani mwa nchi hiyo.

Rasi Mugabe ambae alishindwa na Tsvangirai katika duru ya kwanza ana hofia kuwa huenda mashirika hayo yamekuwa yakimpigia debe mpinzani wake wakati ikigawa misaada.

Mashirika mengi yanaonekana kama yanaushawishi mwingi wa mataifa kigeni kama vile Marekani na Uingereza ambayo yamekuwa yakiukosoa sana utawala wake na kumpendelea Tsvangirai.

Umoja wa Ulaya leo umetoa mwito kwa serikali ya Zimbabwe kuondoa marufuku hiyo.