1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Tuangaliane na tutunzane"

Maja Dreyer17 Aprili 2007

Tayari leo asubuhi, magazeti kadhaa yalitoa uchambuzi wao juu ya mauaji yaliyotokea kwenye chuo kikuu nchini Marekani. Ni habari zinazosikitisha, magazeti yanaandika, lakini majibu kutoka siasa hadi sasa hayafaa.

https://p.dw.com/p/CHTD

Tukianza na gazeti la “Westdeutsche Allgemeine Zeitung”, tunasoma yafuatayo:

“Wanasiasa wamejibu kama ilivyo kawaida. Rais Bush anawapelekea jamaa waliohusika na msimba huo salama zake za rambirambi. Lakini hatua ambayo inapaswa kuchukuliwa sasa ni kubadilisha sheria za silaha. Nchini Marekani ni rahisi kununua silaha kuliko kupata liseni ya kuendesha gari! Katika miaka kumi iliyopita kumetokea mauaji 19 kwenye shule.”

Hivyo linakumbusha gazeti la “Westdeutsche Allgemeine Zeitung”. Mhariri wa “Märkische Oderzeitung” pia anataja wasiwasi juu ya sheria huru ya siasa, lakini suluhisho halipatikani kupitia udhibiti mkali. Ameandika:

“Ni wazi kwamba, majadiliano juu ya upatikanaji huru wa silaha nchini Marekani yatakuwa makali. Lakini sheria hazitabalidishwa. Halafu kutasikika mwito wa kutaka kupigwe marufuku michezo ya video zenye kuonyesha mauaji ya watu. Hiyo pia haitasaidia. Yule ambaye anataka kununua silaha, anaweza kufanya hivyo, hata nchini Ujerumani ambapo sheria ni kali zaidi. Vilevile marufuku dhidi ya michezo ya video hayana maana katika enzi ya mtandao wa Internet ambamo kila kitu kinapatikana bila ya udhibiti. Badala yake sisi binadamu tunapaswa kukaa kwa karibu zaidi, kuangaliana na kutunzana.”

Ni gazeti la “Märkische Oderzeitung” juu ya mauaji ya Marekani yaliyotokea jana. Tukigeuka mada sasa tuyaangalie sasa maonyesho ya kiviwanda ya Hanover ambayo yalifunguliwa mwanzoni mwa wiki hii na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani pamoja na waziri mkuu Tayyip Erdogan wa Uturuki. Sababu ya Ergodan kuwepo ni kwamba Uturuki ni nchi shirika ya maonyesho ya mwaka huu, na ndiyo sababu kuangalia upya mahusiano kati ya Uturuki na Ulaya, kama gezeti la “Volksstimme” la mjini Magdeburg linavyoandika:

“Kabla ya kuwasili Ujerumani, waziri mkuu Erdogan wa Uturuki aliukemea Umoja wa Ulaya. Mjini Hanover lakini pande zote mbili zilijaribu kuonyesha urafiki tena. Kwenye maonyesha ya Hanover, Uturuki inaonekana kuwa nchi yenye ukuaji mzuri wa kiuchumi. Pia mashirika makubwa ya Kijerumani yanajihusisha nchini Uturuki kama vile Siemens, Bosch au Daimler. Kwa hivyo daraja la kiuchumi ni imara, hivyo uwanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya unaweza kujadiliwa upya.”

Na pia gazeti la “Landeszeitung” linasisitiza kuwa Uturuki haina tu umuhimu wa kisiasa:

“Uturuki hasa ni nchi ambapo Uislamu na Demokrasia zinaweza kuunganishwa. Lakini njia ya Uturuki kuingia katika Umoja wa Ulaya imezuiliwa. Kansela wa Ujerumani angeweza kusaidia mradi huu wenye umuhimu katika dunia nzima utekelezwe. Lakini lazime yeye mwenyewe akubali wazo lake la kuipa Uturuki ushirikiano maalum badala la uwanachama halifai.”

Na hatimaye tunaangalia tena kashfa juu ya mkuu wa benki ya dunia, Paul Wolfowitz. Mhariri wa gazeti la “Ostthüringer Zeitung” anachambua njia ya wanasiasa kusonga mbele katika kazi zao kwa ujumla. Ameandika:

“Ebu, inakuaje, Bw. Wolfowitz, ambaye awali alikuwa naibu wa waziri wa ulinzi wa Marekani, alipata cheo hicho? Sababu ni kwamba aliondoshwa kutoka serikalini na alipatiwa cheo hiki. Hivyo ndivyo wanavyofanya Wamarekani, na wengine wote. Ikiwa ni Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa, Shirika la Nato au mashirika mengine ya kimataifa, mara nyingi yanatumiwa kwa kuwapatia nafasi fulani za kazi wanasiasa ambao hawatakiwi tena nyumbani. Hiyo ndiyo kashfa yenyewe. Kwani mashirika haya yanapaswa kuwa na wafanyakazi wa hali ya juu kabisa.”