1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi Ivory Coast

26 Februari 2010

Ivory Coast imeunda tume ya uchaguzi siku chache tu baada ya kuunda serikali na inapoelekea kumaliza mzozo wa kisiasa uliopelekea maandamano makubwa.

https://p.dw.com/p/MDDO
Waandamanaji wasubiri wabunge wapya.Picha: AP

Kulingana na tovuti ya ofisi ya rais, tume hiyo mpya ya uchaguzi ilichaguliwa jana usiku na itaongozwa na Youssouf Bakayoko ambaye ni mwanasiasa wa upinzani.

Laurent Gbagbo
Rais Laurent Gbagbo wa Ivory CoastPicha: AP

Rais Laurent Gbagbo aliivunja serikali ya awali pamoja na tume ya uchaguzi tarehe 12 mwezi huu, uamuzi ambao ulichochea maandamano ya ghasia yaliyosababisha vifo vya watu saba.

Bw. Gbagbo alidai kwamba kiongozi wa tume hiyo ya uchaguzi aliyoivunja alihusika katika mizengwe kwa kuongeza idadi ya wapiga kura wengi kutoka katika kambi ya upinzani.

Waziri mkuu, Guillame Soro, alichukua hatua ya kwanza siku ya jumanne kujaribu kutatua mzozo huo kwa kuunda serikali mpya inayojumuisha vyama vikuu vya upinzani baada ya makubaliano kusimamiwa na rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore, aliyekuwa mpatanishi.

Mwenyekiti wa tume hiyo mpya ya uchaguzi ni Youssouf Bakayoko wa chama cha upinzani cha PDCI.

Bakayoko ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ivory Coast, muda mfupi baada ya kuchaguliwa alisema lengo lao kuu ni kupanga uchaguzi huru na wa haki ili kuwa na matokeo yatakayokubaliwa na kila mtu.

Uchaguzi wa rais ulioahirishwa mara sita tangu mwaka wa 2005 ulipangwa kufanyika mwezi Machi lakini sasa unatarajiwa mwezi Aprili au Mei.

Präsidentenwahl an der Elfenbeinküste Flash-Galerie
Raia wakitafuta majina yao katika daftari la wapiga kura.Picha: DW/ Adayé

Serikali mpya ya Ivory Coast ina wizara ishirini na saba tofauti na thelathini na mbili za zamani.

Jukumu kubwa la tume hiyo mpya ya uchaguzi litakuwa kumalizia kazi ya kuunda orodha rasmi ya wapiga kura, na kuanza kushughulikia majina yaliyokuwa tete katika orodha iliyopingwa na rais Gbagbo.

Wapiga kura milioni sita walikuwa wameandikishwa katika daftari la wapiga kura lakini uraia wa majina milioni moja ulizua ubishi uliochangia vita.

Raia wengi wa Ivory Coast wanadaiwa kuchoka na hali ya vurugu na vita na wana matumaini makubwa kwamba kuteuliwa huko kwa tume mpya ya uchaguzi kutarejesha amani.

Mwenyekiti mpya wa tume hiyo, Youssouf Bakayoko, alisema taasisi yao ilikumbwa na changamoto nyingi za kutekeleza majukumu na akaapa kwamba tume mpya itajizatiti ili iaminiwe na raia wa Ivory Coast.

Ivory Coast imegawanyika kati ya kaskazini inayomuunga mkono waziri mkuu Guillaume Soro aliyekuwa kiongozi wa waasi, na raia wa kusini wanaomuunga mkono rais Laurent Gbagbo aliyeponea chupuchupu jaribio la mapinduzi dhidi yake mwaka wa 2002 lililochangia vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wachunguzi wa kisiasa nchini humo wanadai kwamba kuundwa kwa tume mpya ya uchaguzi ni jambo la muhimu zaidi kuliko kuundwa kwa serikali ambayo ni ya mpito, kulingana na mkataba wa 2005 ambao umepitwa na wakati.

Wanadai kwamba uchaguzi ndio njia ya pekee ya kumaliza mzozo wa kisiasa katika nchi hiyo inayosifika duniani kwa uzalishaji wa kakao.

Mwandishi: Peter Moss/DPA/Reuters

Mhariri:Othman Miraji