1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya uchaguzi Zimbabwe yachelewesha kutangaza matokeo ya urais

Kalyango Siraj2 Aprili 2008

Tsvangirai atishia kutangaza matokeo yake

https://p.dw.com/p/DZC8

Matokeo ya uchaguzi wa Urais uliofanyika mwishoni mwa juma hadi sasa hayajatolewa.Kwa mda huohuo upande wa upinzani unaongoza upande wa serikali katika uchaguzi wa viti vya ubunge.

Kiongozi wa upinzani Morgen Tsvangirai,amekataa kujitanganza mshindi akisema anasubiri kutangazwa kwa matokeo rasmi.

Matokeo ya uchaguzi wa Urais nchini Zimbabwe hayajatolewa rasmi hadi kufikia sasa.Na shinikizo limeongezeka leo jumatano la kuitaka tume ya uchaguzi kutoa matokeo hayo.Gazeti la serikali ya Zimbabwe la The Herald linabashiri kuwepo duru ya pili katika king'ang'anio cha kiti cha urais.

Upande wa upinzani inadai umeshinda uchaguzi huo na kutishia kuchapisha takwim zao zikionyesha ushindi ikiwa hatua hazitachukuliwa kuchapuza kutoa matokeo.

Duru za tume ya uchaguzi nchini humo zinasema kuwa matokeo ya mwisho ya viti vya bunge yatatolewa baadae leojumatano.Lakini inasemekana tume hiyo imetakata kutoa ratiba ya kutoa matokeo ya urais.Lakini matokeo yasio rasmi yanaonyesha kama Tsvangirai akiwa mbele ya rais Robert Mugabe,lakini sio kiwango cha kumuwezesha kuepuka duru ya pili.

Kuhusu viti vya ubunge, kwa mujibu wa shirika la habari la kifaransa la AFP inasemekana chama cha upinzani cha MDC cha Tsvangirai kina viti 96 huku chama cha rais Mugabe ZANU PF viti 91.

Hesabu hizo zilitegemea matokeo ya ubunge kutoka majimbo 188 kati ya majimbo ya uwakilishi 210.

Gazeti la serikali la The Herald, lilikuwa limetabiri kabla ya uchaguzi kuwa Mugabe atambwaga Tsvangirai,kwa kupata 57% ya kura na kusema kuwa Tsvangirai angweza kupata 27% ya kura.

Lakini sasa limebadili kauli yake katika toleo la leo jumatano. Gazeti hilo limetabiri kuwa Mugabe ataingia duru ya pili mwezi huu.

Liki mnukuu mchambuzi mmoja aliesema kuwa,mwelekeo wa matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu unaonyesha uwezekano wa kupatikana kwa duru ya pili kwani hakuna mgombea atakaeweza kupata 51%.

Tsvangirai ambae alishindwa na Mugabe miaka sita iliopita kwa kile anchodai kuwa kulifanyika mizengwe,anaaamini kuwa mara hii ushindi ni wake lakini amekataa kujitangaza mshindi akisubiri matokeo ya mwisho ya tume ya uchaguzi ambayo imechelewesha matokeo.

Hali hiyo sio tu inatia wasiwasi miongoni mwa raia wa Zimbabwe lakini pia na wa mataifa ya kigeni.

Naibu msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Marekani,Tom Casey,amewambia maripota kuwa wanatiwa wasiwasi na kutotangazwa kwa matokeo na wanahisi kuwa hatua hiyo haileti matumaini.

Duru za kidiplomasia mjini Pretoria, Afrika Kusini zinazungumzia rais wa nchi hiyo Thambo Mbeki kuwasiliana na mwenzake wa Marekani George W. Bush pamoja na waziri mkuu wa Uingereza,Gordon Brown, kumshauri mwenzake Mugabe kuupiga moyo konde.

Mugabe hajaonekana hadharani tangu jumamosi, na pia kuna uvumi eti anashinikizwa kung'atuka, madai yaliyokanushwa na upande wa Mugabe.

Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini amenukuliwa na vyombo vya habari vya nchi za nje akisema kuwa anaunga mkono juhudi zozote ambazo zinaweza kusaidia kumaliza mgogoro wa Zimbabwe.